KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Juma Mwambusi amesema wiki mbili zimetosha kukaa na wachezaji wa timu hiyo na kuunda upya mikakati yao, baada ya kuanza na kikosi hicho katikati ya msimu huu tena kikiwa tayari kiko kwenye mechi za kiushindani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwambusi alisema katika kipindi cha michezo ya kimataifa kimesaidia kukaa vizuri na wachezaji na kuunda mikakati mipya kwa ajili ya msimu huu, kwani kabla ya hapo hawakuwa na muda bora kutokana na ufinyu wa ratiba.
“Nafikiri sasa ninaweza kuzungumza chochote kwa sababu nimekaa na wachezaji kwa muda mrefu kidogo kama ndio tupo kwenye maandalizi ya msimu ‘Pre Season’, maendeleo ya mmoja mmoja ni mazuri na wameonyesha morali ya kuipigania timu,” alisema.
Mwambusi alisema katika kipindi chote cha mapumziko alikuwa na kazi ya kuboresha maeneo mawili muhimu ndani ya timu hiyo akianza na eneo la ulinzi na lile la ushambuliaji, kwani kwenye michezo 11 waliyocheza wamekosa uwiano mzuri kiuchezaji.
“Tumecheza michezo 11 ingawa mingine nimeikuta wameshacheza, tumefunga mabao tisa na tumeruhusu 10, sasa hii inaonyesha wazi hatuko sehemu salama katika maeneo hayo mawili, sio kazi ya siku moja hivyo tutarekebisha kadri ambavyo tuwezavyo.”
Mwambusi amejiunga na kikosi hicho Oktoba 23 mwaka huu, baada ya kukaa nje kwa muda mrefu tangu Februari 12, 2023 alipoachana na Ihefu ambayo sasa inafahamika kwa jina la Singida Black Stars, akichukua nafasi ya Mkenya, David Ouma aliyetimuliwa Agosti 24.
Mchezo wa kwanza kwa kocha huyo alianza kwa kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Yanga Oktoba 26, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, akashinda bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar Oktoba 29, kisha suluhu na Singida Black Stars Novemba 2.
Kikosi hicho kitapambana na KenGold kesho katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, huku timu hiyo ikishika nafasi ya 10 na pointi zake 12, baada ya kushinda michezo mitatu, sare tatu na kupoteza mitano.