Kampuni ya Vodacom Tanzania Plc imetembelea soko la Makumbusho jijini Dar es Salaam kutoa elimu na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu utapeli wa kimtandao. Zoezi limefanywa kwa lengo la kuwasaidia watumiaji wa mtandao namna ya kutambua na kuepuka matapeli katika mitandao ya simu.
“Tatizo la utapeli wa mtandaoni limekuwa likiongezeka kila siku ambapo watu wengi wamekuwa wahanga kwa kupoteza fedha zao bila kujua nini cha kufanya. Hivyo Vodacom tumekuja leo kutoa elimu na kuongeza uelewa kwa wananchi ili wajue jinsi ya kukubaliana na matapeli,” anasema Agapinus Tax, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Hatari na Utii wa Sheria kutoka Vodacom Tanzania.
Agapinus anasema hili zoezi ni endelevu na litakuwa pia katika mikoa ya Rukwa na Morogoro ambayo, kwa mjibu wa takwimu, ni kati ya mikoa inayoongoza kwa vitendo vya utapeli wa mtandaoni.