MKURUGENZI GEITA DC AWASHUKIA WAZABUNI WANAOKWAMISHA MIRADI

Na Nasra Ismali, Geita

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ndg Karia Magaro Novemba 18, 2024 ameongoza timu ya menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya Geita kukagua miradi ya maendeleo katika kata za Nyamigota, Ludete na Katoro zilipo jimbo la Busanda.

Timu hiyo imetembelea na kukagua ujenzi wa shule ya amali iliyopo kata ya Nyamigota kijiji cha Chibingo mradi wenye thamani ya Shilingi Milioni 584,280,029 ili kuona hali halisi ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Aidha timu ya menejimenti imetembelea mradi wa upanuzi wa miundombinu ya kidato cha 5 na 6 shule ya sekondari Kagega wenye thamani ya shilingi Milioni 481, upanuzi wa miundombinu ya kidato cha 5 na 6 shule ya sekondari Lutozo mradi wenye thamani ya shilingi Milioni 381 na mradi wa shule ya msingi mtaa wa afya ambayo ilianza kwa nguvu za wananchi na baadaye kuendelezwa madarasa 9 kwa mfuko wa BOOST kwa thamani ya Milioni 351.5.

Pamoja na miradi hiyo, timu iliweza kutembelea Kata ya Katoro eneo ambalo litajengwa shule ya sekondari ya kata ambapo kwa sasa ipo hatua za awali. Mradi huo una jumla ya kiasi cha shilingi Milioni 584,280,029.

Katika ukaguzi wa miradi hiyo timu ilibaini kuwepo kwa changamoto zinazosababishwa na wazabuni kwa kuchelewesha vifaa vya ujenzi kwenye miradi na hii ni kutokana na wazabuni hao kushinda tenda katika maeneo mengi ilihali hawana uwezo wa kusambaza vifaa kwa wakati.

Kufuatia changamoto hiyo, timu ya menejimenti iliwafuatilia wazabuni hao na kuwapa muda maalum wa kuhakikisha vifaa vya ujenzi vinafika kwenye miradi ili mafundi ujenzi waweze kuendelea na kazi na miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuanza kutumika kama ambavyo mikataba ya ujenzi inavyowataka.
“Hizi kazi ni za Halmashauri hivyo niwatake mnapotangaza tenda kwenye mfumo wa Nest muangalie uwezo wa wazabuni katika kukamilisha kazi wanazoziomba katika Halmashauri ili kuepusha kuchelewesha miradi” amesema Magaro .

Fundi Deogratius Wilson ni mmoja wa mafundi wanatekeleza miradi iliyotembelewa na timu ya menejimenti ambapo amesema wanatumia muda mwingi kuwepo uwandani (site) bila ya kuwepo kwa madini ujenzi kutokana na wazabuni kutokupeleka vifaa kwa wakati jambo ambalo lina wagharimu katika kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.

Kwa upande wake Scolastika Vitalis ambaye ni mmoja wa wanakamati wanaosimamia miradi ameileza timu ya menejimenti adha wanayoipata kutokana na wazabuni kutokusambaza madini ujenzi kwa wakati na kuwafanya kukaa uwandani(site) bila kazi yoyote.

Kufuatia changamoto hizo Ndg Magaro ametoa maagizo mazito kwa wazabuni hao ikiwa ni pamoja na kufika kwenye ofisi zao akiwa na timu ya menejimenti na kuwataka kusambaza vifaa kama ambavyo mikataba yao ipo na iwapo watashindwa basi mikataba yao itaenguliwa na kazi hizo kupewa wazabuni wengine.

Pamoja na hayo Mkurugenzi amewataka walimu ambao wana simamia miradi hiyo kuhakikisha ubora wa vifaa vinavyoletwa na wazabuni hao vina ubora unaostahili ikiwa ni pamoja kusimamia kila hatua ya ujenzi kwa kushirikiana na kutoa taarifa mahali penye changamoto ili miradi isisimame na wanafunzi waweze kuitumia ifikapo mwakani.

Huu ni utaratibu unaofanywa na Mkurugenzi Mtendaji kwa kushirikiana na timu ya menejimenti kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuendelea kuweka msukumo katika ukamilishwaji wake
Halmashauri ya wilaya ya Geita inaendelea kuishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuleta fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali ya Maendeleo.



Related Posts