Dar es Salaam. Shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka katika kesi ya kuwepo nchini bila kuwa na kibali inayomkabili raia wa Burundi, Ferdnand Ndikuriyo (27) maarufu Chuma cha Chuma, ameieleza Mahakama kuwa mshtakiwa alishawahi kuwa na kesi kama hiyo Mahakama ya Mwanzo Kinondoni.
Amedai katika kesi hiyo alihukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita, akielekezwa na Mahakama aende Polisi kuchukua hati yake ya kusafiria ili aipeleke Uhamiaji kuhuisha kibali cha kuishi nchini, jambo ambalo hakulitekeleza wala hakuwahi kurudi Polisi hadi alipokamatwa tena.
Shahidi huyo, F 4381 Sajenti Philipo Warioba (49) kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni, ametoa ushahidi leo Novemba 21, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Chuma ambaye ni msanii wa muziki na makazi yake ya muda ni Mbezi Louis, alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Novemba 4, 2024 na kusomewa shtaka hilo.
Akiongozwa kutoa ushahidi na Wakili wa Serikali, Raphael Mpuya, mbele ya Hakimu Yusto Ruboroga, Sajenti Warioba amedai Desemba 12, 2022 akiwa Kituo cha Polisi Oysterbay alipokea jalada la polisi lenye kumbukumbu namba IR 7827 la mwaka 2022 lililokuwa na kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, mshtakiwa katika shauri hilo alikuwa Ferdnand Ndikuriyo maarufu kama Chuma.
“Mshtakiwa alikuwa anakabiliwa na kosa la kujipatia fedha kwa njia ya uchunguzi, hivyo alikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Oysterbay,” amedai.
“Baada ya kukamatwa Ndikuriyo, nilipewa jalada lile kwa ajili ya kulifanyia uchunguzi mimi na mwenzangu ambaye kwa sasa amehamishwa,” amedai shahidi.
Ameeleza walienda kufanya upekuzi katika makazi ya mtuhumiwa ambako walikuta hati ya kusafiria ya kwake na za raia wengine wa Burundi.
“Pasipoti yake ilibainika imeisha muda wake wa kutumika, hali hiyo ilisababisha mshtakiwa afunguliwe kesi nyingine ya kuishi nchini bila kuwa na kibali,” amedai.
Ameeleza alifunguliwa jalada la polisi Novemba 9, 2023 kosa lilikuwa kuishi nchini bila kuwa na kibali.
Baada ya upelelezi kukamilika, amedai mshtakiwa alifikishwa Mahakama ya Mwanzo Kinondoni alikosomewa kesi ya jinai namba 83 ya mwaka 2023 yenye shtaka la kuishi nchini bila kuwa na kibali, mbele ya Hakimu Mushi.
“Katika kesi hiyo, mshtakiwa alikiri shtaka na alihukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita,” amedai na kueleza pia Mahakama ilimuelekeza aende Idara ya Uhamiaji akarekebishe nyaraka zake, ikiwemo kuomba kibali cha kuishi nchini ili aishi vizuri.
“Baada ya hukumu kuelekeza hayo, mshtakiwa hakufuata maelekezo wala hajawahi kuja Polisi Oysterbay kufuata hati yake ya kusafiria,” amedai.
Amedai hati hiyo ya kusafiria iliendelea kubaki kituoni hapo.
Shahidi alidai Septemba 2024, mshtakiwa alikamatwa na alimkuta mahabusu ya Oysterbay.
Amedai mshtakiwa alikamatwa kutokana na kutafutwa na ubalozi wa nchi yake.
Sajenti Warioba baada ya kuhitimisha ushahidi aliulizwa maswali baadhi yakiwa kama ifuatavyo:
Mshtakiwa: Mlivyonikamata kwa nini hamkunipeleka Uhamiaji?
Shahidi: Tulikuwa tunaendelea na uchunguzi na baadaye ulipelekwa.
Mshtakiwa: Unasema mlinikamatia wapi?
Shahidi: Mimi sijakukamata, mimi nilipewa jalada la Polisi nilifanyie uchunguzi.
Hakimu alimuuliza shahidi kwa nini hawakumpatia hati yake ya kusafiria mshtakiwa baada ya kuhukumiwa kifungo cha nje?
Shahidi: Mheshimiwa hakimu, mshtakiwa hakuwahi kurudi Polisi kuja kuchukua hati yake ya kusafiria na pale Polisi alikuwa na vitu vyake vingine kama vile Laptop, lakini hakuwahi kurudi.
Shahidi: Ndiyo mheshimiwa, tulimtafuta kwa sababu kwenye jalada kuna namba zake za simu, lakini hazikupatikana na hazijawahi kupatikana mpaka sasa.
Hakimu: Kwake mlikwenda? Maana si ulisema wakati wa upelelezi mlikwenda kufanya upekuzi?
Shahidi: Ndiyo kwake tulikwenda, lakini hatukumpata kwa sababu alihama eneo hilo.
Alipoulizwa na upande wa mashtaka sababu za kumkamata mshtakiwa kwa mara ya pili ni zipi alijibu:
Shahidi: Ni za kuishi nchini bila kuwa na kibali, lakini pia kulikuwa na taarifa kuwa anatafutwa na ubalozi wa nchi yake.
Kesi hiyo itaendelea leo Novemba 22 kwa shahidi wa pili kutoa ushahidi.