Mchuano wa sera vyama vikitafuta kura za viongozi

Dar/mikoani.  Wakati kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji zikiwa zimeanza, vyama vimeendelea kunadi sera zake ili kuwashawishi Watanzania  kuwapigia kura wagombea katika uchaguzi utakaofanyika Jumatano ya Novemba 27, 2024.

Vyama hivyo vimewasisitiza Watanzania kuchambua sera na vipaumbele vya wagombea  ili kufanya uamuzi wa kuchagua viongozi sahihi watakaowahudumia katika kipindi cha miaka mitano.

Kampeni hizo zimeendelea katika mitaa, vijiji na vitongoji kwenye mikoa mbalimbali nchini zikiongozwa na viongozi na watendaji wakuu wa vyama vya siasa.

Miongoni mwa vyama hivyo ni Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT- Wazalendo na Chama cha Wananchi (CUF).

Akizungumza na wananchi wa Nyamongo mkoani Mara, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (bara), Tundu Lissu amewataka wananchi kuwapigia kura wagombea wao waliobakia baada ya wengine kuenguliwa kwa sababu mbalimbali ikiwamo makosa ya kukosea majina na herufi.

“Kazi ya kwanza ni kuhakikisha wote wanaingia kwenye ngazi ya halmashauri wanashinda kwenye vitongoji, vijiji, mitaa na halmashauri tukiwa na wawakilishi wengi katika vijiji na vitongoji sisi tutakuwa na uamuzi,” amesema Lissu  ambaye ni mbunge wa zamani wa Singida Mashariki.

Amesema wakifanikiwa kushinda, watakuwa na nguvu ya kwenda kutibu vilio vya kila aina vinavyowakabili wananchi kwa zaidi ya miaka 20 na kupata haki zao.

“Tutakuwa na uwezo wa kuhoji na kudai haki itendeke kwa wote ambao ndugu zao, wamejeruhiwa, kufungwa, kunyang’anywa mashamba na nyumba zao tutakuwa na uwezo wa kusema,” amesema Lissu.

Kiongozi wa zamani wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amewataka wananchi kuchagua viongozi wanaowajibika na kushughulika na shida zao zinazowakabili ili kupata ufumbuzi wa kudumu.

Zitto ambaye ni mbunge wa zamani wa Kigoma Mjini ameeleza hayo wakati akihutubia katika mikutano ya hadhara aliyoifanya mikoa ya Tabora na Kigoma Kusini, akieleza kuwa, ilani ya ACT-Wazalendo imeweka bayana mgombea wao akishinda uenyekiti, watafanya mikutano ya kijiji.

“Tutawarudishia sauti ya vijiji vyenu kila baada ya miezi mitatu lazima kuwe na mkutano mkuu wa  kijiji wa kujadili mambo yenu,” amesema Zitto.

Hoja hiyo imeungwa mkono na mwenyekiti wa zamani wa ACT- Wazalendo, Juma Duni Haji maarufu Babu Duni na kuwataka wananchi kuwaondoa viongozi wote wanaojiona miungu watu.

“Nchi hii inamilikiwa na ninyi wananchi na nawaambia hakuna mwenye nguvu kuwashinda, tatizo lenu ni mnajipa uoga na maisha yenu yanaathiriwa zaidi na siasa kikubwa jitokezeni kuwaondoa,” amesema Duni ambaye ni mwanasiasa mkongwe.

Duni amesema hayo alipozungumza na wananchi wa Mtaa wa Tupendane, Kata ya Manzese katika Jimbo la Ubungo mkoani Dar es Salaam.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesema hatua ya wajumbe wa kamati kuu na halmashauri kuu ya chama hicho, kushiriki katika uzinduzi wa kampeni hizo imekuwa matokea chanya kwa makada wa upinzani kujiunga na chama hicho tawala.

Makalla  amesema hayo wakati akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Mzimu wilayani Kigamboni katika mwendelezo wa ziara ya kuwanadi na kuwaombea kura wagombea wa uenyekiti wa mitaa katika mkoa wa Dar es Salaam.

“Kishindo cha wajumbe wa kamati kuu na halmashauri kuu, naomba nitoe taarifa kwamba kampeni zetu zimekwenda vizuri jana (Jumatano) na kishindo cha jana kimefanya wapinzani kuhamia CCM.

“Tumekuwa na mikutano mikubwa yenye hamasa ya watu wenye imani na Chama cha Mapinduzi, naongea kwa kujiamini kwamba uzinduzi wa jana umetoa dira na matumaini makubwa kwa wagombea wa CCM kuibuka kidedea,” amesema Makalla.

Makalla amesema CCM itashinda kwa kishindo wakati baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani, akiwataka Watanzania kutopata shida katika kufanya uamuzi sahihi wa kukipa kura chama hicho tawala.

“Viongozi wa CCM ikifika Novemba 24 wakumbusheni majirani zenu na ndugu zako kupiga kura, usikubali kuambiwa kwamba CCM imeshinda bali hakikisha watu wanapiga kura ili tupate ushindi wa kishindo,” amesema Makalla.

Katika hatua nyingine, Makalla amesema,”naomba mtuchagulie wagombea wa CCM kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa na watangulizi, msituchanganyie tunataka watu wanaogusa maendeleo ya wananchi.” Katibu wa (CCM) Wilaya ya Kibaha Vijijini mkoani Pwani, Stevin Shija amesema chama hicho, hakitawafumbia macho wasaliti wakati wa uchaguzi wa Serikali za mitaa badala yake kitawavua uanachama.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni zilizofanyika Kijiji cha Dutumi amesema,”tumebaini katika maeneo fulani tumekosa uongozi, si kwa sababu hatupendwi, bali baadhi ya wanachama wetu wameshindwa kwenye kura za maoni.”

“Sasa badala ya kukubali kushindwa, wamejipa jukumu la kuharibu mchakato,” amesema Shija.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), January Makamba akizungumza kwenye mikutano ya Jimbo la Bumbuli, mkoani Tanga, amesema kushughulika na kero zinazowakabili wananchi ni turufu ya chama hicho kushinda katika uchaguzi huo.

“Wagombea  wote tuliowateua  kwa nafasi hizi za uenyeviti ni muhimu wakazingatia dhima hiyo na dhamira hiyo na waelewe  kwamba CCM  ndio imeasisi  mfumo wa  utawala wa  kugatua na kuleta  madaraka  kwa wananchi na  nguvu ya mamlaka makubwa  imepelekwa kwenye  Serikali za mitaa,”amesema Makamba.

Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), maarufu mzee wa ‘ubwawa’ Hashim Rungwe amesema kampeni zao za kishindo wanatarajia kuzindua kuanzia kesho Ijumaa maeneo ya Kijitonyama wilayani Kinondoni.

“Kampeni zetu zitakuwa za tofauti na ajenda yetu kubwa wananchi wachague viongozi wanaofaa ili kuwasaidia wakati wa shida na raha tofauti na ilivyo sasa,” amesema Rungwe akizungumza na Mwananchi.

Mgombea wa nafasi ya uenyekiti Mtaa wa Tandika wilayani Temeke kwa tiketi ya CUF,  Salehe Mahimbo, jana akiomba kura kwa wananchi wa mtaa huo, amesema akichaguliwa nafasi ataweka utaratibu mzuri wa ukusanyaji taka na kuondoa kero ya ulinzi shirikishi.

“Kuondoa unyanyasaji na uonevu kwa kila mtu bila kujali chama anachotoka na kuunganisha wananchi kwa kutengeneza dawati la kujadili mambo yetu,”amesema Mahimbo miongoni mwa sera atakazinadi na kuzisimamia katika kampeni zake.

Wakati vyama vikiendelea kujinadi, Jeshi la Polisi limesema litaimalisha ulinzi wakati wote kabla na baada ya uchaguzi huku Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) likionya vitendo vya rushwa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Songwe, Augustino Senga akizungumza na waandishi wa habari kwenye mafunzo maalumu kuelekea uchaguzi huo, amesema uchaguzi huo ni tukio muhimu kwa Taifa.

“Uchaguzi ni kipindi muhimu kinachowahusisha wananchi kutimiza haki zao za kidemokrasia, ikiwamo kujiandikisha, kugombea, kusikiliza wagombea, kuchagua na kuchaguliwa,” amesema Senga.

Takukuru Temeke jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na Chama cha Madereva na wamiliki wa bajaji na bodaboda (CMPD) Mkoa wa Dar es Salaam, imewataka baadhi ya wagombea wa uchaguzi huo kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa hiari.

Mkuu wa Takukuru, Temeke Ismail Bukuku amesema,“ubandikaji wa vipeperushi kwenye bodaboda ni njia moja wapo ya kufikisha jumbe za kupinga rushwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa.”

Katibu wa CMPD Mkoa wa Dar es Salaam, Judica Pallagyo amesema chama hicho si  sehemu ya kuendekeza rushwa.

“Tumefanya kazi na Takukuru kwa ushirikiano na kwa  muda mrefu, tunaahidi kushiriana kikamilifu na taasisi hii kupinga vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na hata uchaguzi wa 2025,”amesema Pallagyo.

Related Posts

en English sw Swahili