Bumbuli. Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), January Makamba ameyataja mambo yatakayokibeba Chama Cha Mapinduzi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Makamba amesema namna chama hicho kinavyoshughulikia na kuzipatia ufumbuzi kero zinazowakabili wananchi katika maeneo mengi nchini yanaipa CCM nafasi ya kufanya vizuri katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Ameyataja mambo hayo kuwa ni ubora wa wagombea, ubora wa sera, ubora wa vyama na rekodi ya uongozi.
Makamba ameyasema hayo leo Alhamisi Novemba 21, 2024 alipokuwa akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM katika mikutano ya kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa ziliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli.
Amesema mambo hayo manne, ndiyo yanayokibeba chama hicho alichosema kitashinda uchaguzi huo katika maeneo mengi kutokana na rekodi yake.
“Ninasema haya kwa sababu nina uhakika wa ushindi wa CCM unaotokana na namna inavyoshughulikia na itakavyoendelea kuzishughulikia na kuzimaliza changamoto zinazowakabili wananchi,” amesema mbunge huyo huku akiwahamasisha wananchi kuwachagua viongozi wanaowania kwa tiketi ya chama hicho.
Amesema wajibu wa CCM siku zote si kujihangaisha na siasa za ndani ya vyama vya wapinzani, bali kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa na imani nacho.
“Siku zote chama na sisi viongozi wake tutaendelea kuwasemea na kuwatetea wananchi. Bila hivyo, hata upinzani ukipasuka vipi kama wenyeviti wetu wa serikali za vijiji wanawapuuza na kuwakera wananchi, ushindi wa CCM utakuwa hatarini.
Amesema wagombea wote walioteuliwa na CCM kuwania nafasi za wenyeviti ni muhimu wakazingatia dhima hii na dhamira hii ya chama na waelewe kwamba chama chao ndio kimeasisi mfumo wa utawala wa kugatua na kuleta madaraka kwa wananchi,” amesema Makamba.
Amesema nguvu na mamlaka makubwa imepelekwa kwenye serikali za mitaa ikiwamo uamuzi unaohusu ustawi na maendeleo ya wananchi katika maeneo yao.
Hivyo amesema viongozi wanaochaguliwa katika uchaguzi huu wajue kwamba wana umuhimu mkubwa katika suala zima la uongozi wa nchi hii.
“Watu mara nyingi wanaamini uchaguzi huu ni wa daraja la pili na kwamba, uchaguzi ule unaoitwa mkuu ndiyo muhimu zaidi, dhana hiyo haikuwa sawa,” amesema Makamba.
Amesema uchaguzi huu una nguvu ya kipekee kwa kuwa unachagua viongozi muhimu wanaoishi na wananchi katika maeneo yao.
Hivyo, amesisitiza kuwa CCM ina mfumo mzuri wa kuwapata wagombea kwa sababu wagombea wanateuliwa na halmashauri kuu za wilaya ambayo ni kundi la watu wengi, hawawezi kufanya makosa kwenye kuwapata wagombea hao.
Hata hivyo, Makamba alimewaomba wananchi na wanaCCM Novemba 27, 2024 kujitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura na kukichagua Chama cha Mapinduzi kwa maendeleo ya nchi.