Fadlu Davids aweka mtego Ligi Kuu Bara

SIMBA waliitaka mechi ya leo dhidi ya Pamba Jiji na wamepatiwa baada ya hapo awali Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuitoa katika tarehe iliyopangwa ili kuipa nafasi zaidi timu hiyo kujiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi dhidi ya Bravos.

Kocha mkuu wa Simba, Fadlu Davids aliona kukaa wiki mbili bila ya kucheza mechi ya kimashindano inaweza kumpa wakati mgumu zaidi kwenda kukabiliana na Bravos Novemba 27 mwaka huu, hivyo uwepo wa mchezo wa leo dhidi ya Pamba Jiji, kwake imekuwa poa sana.

Simba ambao ni vinara wa Ligi Kuu Bara, leo watakuwa wageni wa Pamba Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuanzia saa 10 jioni.

Ni mchezo uliokaa kimtego zaidi kutokana na aina ya timu zinazokwenda kukabiliana huku kila mmoja akihitaji pointi za kumuweka sehemu nzuri zaidi katika msimamo.

Simba yenye pointi 25 kileleni mwa ligi baada ya kucheza mechi 10, inahitaji kushinda leo ili kutanua wigo wa pointi dhidi ya wanaomfuatia wakiwamo Yanga wenye 24, Singida Black Stars (23) na Azam (21).

Mbali na ishu ya pointi, uamuzi wa Simba kuucheza mchezo huo ni sehemu ya maandalizi ya kwenda kuikabili Bravos lakini pia inafahamu kwamba wapinzani wao hao watakuwa wakiwafuatilia.

Katika kulitambua hilo, kuna uwezekano mkubwa kikosi cha Simba leo kikawa na mabadiliko ambayo yatatumika kuwavuruga Bravos wasielewe, lakini pia hata aina ya uchezaji inaweza kubadilika.

Fadlu ambaye amekuwa akiwatumia zaidi mabeki Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ nafasi za pembeni kulia na kushoto huku Che Malone Fondoh na Chamou Karaboue pale katikati, leo anaweza kuwashangaza wengi.

Hiyo inatokana na kwamba Kapombe na Tshabalala kutokuwa na timu kwa takribani wiki mbili wakiwa wamekwenda kuitumikia Taifa Stars kwenye mechi za kufuzu Afcon 2025, hivyo anaweza kuwapumzisha au kuwapa muda mchache wa kucheza na kuwatumia Kelvin Kijili au David Kameta upande wa kulia, wakati kushoto akicheza Valentine Nouma.

Mbali na hao, pia kipa Moussa Camara aliyekuwa na kikosi cha Guinea ambaye ndiye kipa namba moja wa Simba akicheza mechi zote kumi, uwezekano wa kucheza upo, lakini pia uwepo wa Ally Salim na kurejea kwa Ayoub Lakred inaweza kuwa sapraizi nyingine golini leo.

Fadlu amesema Kapombe, Tshabalala, Kibu Denis na Camara wamejiunga na timu juzi na jana walitarajiwa kufanya mazoezi binafsi ya kurejesha utimamu huku mshambuliaji, Steven Mukwala akitarajiwa kuungana na wenzake jana Alhamisi jijini Mwanza.

“Maandalizi yameenda vizuri baadhi ya nyota wa kimataifa wamerudi jana (juzi) na wamefanya recovery (kuondoa uchovu) na leo (jana) pia watafanya hivyo, tuko tayari kwa mechi, kipaumbele tunakiweka kwa hao 18 waliokuwapo kwa kuwapa mbinu na kuwatumia kwenye mchezo kama huu.

“Tumeshafanya maandalizi na wachezaji waliokuwapo nadhani hawa waliokuja tutatumia muda huu kutoa maelekezo ya kile tulichokifanya na nini tunachotaka kukifanya katika mchezo wa kesho,” alisema Fadlu.

Katika msafara wa wachezaji wa Simba ulioondoka Dar juzi usiku kwenda Mwanza kucheza mechi hiyo, kiungo mkabaji Yusuph Kagoma na winga Joshua Mutale waliachwa kwa sababu ya kutokuwa fiti.

Fadlu amesema: “Hatuna sababu za kulazimisha wawepo kwenye mipango ya timu wakati tuna michezo mingine mingi mbele, hivyo tunahitaji kuwa na wachezaji walio fiti kwa asilimia zote, Kagoma na Mutale tunataka wawe vizuri kabisa ndiyo wajumuishwe kikosini.”

Wakati Simba ikiwa hivyo, upande wa Pamba Jiji iliyotoka kuifunga Fountain Gate ugenini katika mchezo wa mwisho uliochezwa Novemba 5 mwaka huu, imeshasema kwamba inahitaji kuwa na mwendelezo huo mzuri wa ushindi.

Pamba Jiji iliyorejea Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kupita takribani miaka 23, haina matokeo mazuri kwani katika mechi 11 ilizocheza imeshinda moja pekee, ikitoka sare tano na kufungwa tano.

Tangu ujio wa kocha Fred Felix Minziro akichukua mikoba ya Goran Kopunovic, kuna matumaini yameonekana huku wakishinda mchezo wao wa kwanza wa ligi.

Minziro ambaye ameiongoza timu hiyo katika michezo minne, alianza na sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Kagera Sugar, kisha kufungwa mbili mfululizo ugenini dhidi ya Tabora United (1-0) na Namungo (1-0), kabla ya kushinda 1-0 ugenini mbele ya Fountain Gate.

“Tumekuwa tukipambana baada ya kupata ushindi mchezo uliopita walau presha imepungua, kwa hiyo tunakwenda kwenye mchezo huu bila presha na tunategemea mchezo mzuri.

“Nimepata muda wa kujiandaa vizuri, kukielewa na kukifahamu vizuri kikosi chetu kwa kuwaelewa wachezaji mmoja mmoja, tumefanya masahihisho mengi kuanzia ulinzi mpaka ushambuliaji. Mimi naamini kama wachezaji watafuata maelekezo yetu na kujituma basi tutapata matokeo mazuri,” alisema kocha huyo.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa Mei 14, 2022 katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mchezo wa leo unatarajiwa kuchezeshwa na mwamuzi wa kati Katanga Hussein kutoka Tabora, akisaidiwa na Abdulaziz Ally (Arusha) na Athuman Rajabu (Kigoma) huku mwamuzi wa akiba ‘Fourth Official’ akiwa Ludovic Charles (Mwanza).

Related Posts