WAOGELEAJI 49 kutoka Tanzania na viongozi tisa wameenda nchini Burundi kushiriki mashindano ya Afrika Kanda ya Tatu yanayotarajiwa kuanza kesho Ijumaa hadi Jumapili huku wakiahidi kurudi na ushindi.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Michael Livingstone alisema maandalizi ya kikosi hicho yako vizuri kwani wamekuwa wakijifua kwa muda mrefu kwaajili ya mashindano hayo ambayo anaamini ushiriki wao utaliheshimisha taifa.
“Kazi yetu kama walimu tumeifanya kwa usahihi, kilichobaki ni wachezaji kufanya kazi yao kwa usahihi, naamini kwa ubora wa wachezaji wangu tutafanya kitu kizuri na kuiwakilisha vizuri nchi kwenye michuano hiyo,” alisema.
Nahodha wa timu hiyo, Colins Saliboko ameahidi watarejea na ushindi akisema maandalizi waliyoyapata kutoka kwa makocha wao yanawapa nafasi ya kujiamini.
“Tunaenda kushindana, tulichofundishwa tunatakiwa kukifanya kwa vitendo bila kujali tunakutana na mpinzani wa aina gani, matarajio yetu ni makubwa,” alisema Saliboko.
Ofisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Charles Maguzu amewataka waogeleaji hao kutumia mashindano hayo kuliheshimisha Taifa kwa kufanya vizuri.
“Hakikisheni mnashindana kwa moyo mmoja huku mkiwa na kumbukumbu kuwa mnalipambania taifa kama wapiganaji kulinda heshima ya taifa letu, tunawaamini na tunatarajia mtafanya vizuri,” alisema.
Maguzu ameishukuru Kampuni ya Great Lake Zone kwa kuigharamia timu hiyo kwenda nchini Burundi huku akisema hatua hiyo ni namna mojawapo ya kuiunga mkono Serikali katika jitihada zake za kuinua michezo nchini.