Vigezo aliyejifungua kwa upasuaji kuzaa kawaida

Dar es Salaam. Kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ya uzito mkubwa kwa mtoto, inaelezwa kuwa husababisha daktari kumshauri mjamzito kujifungua kwa njia ya upasuaji.

Hata hivyo, baadhi ya wanawake mara nyingi hufikiria kwamba akijifungua kwa upasuaji, basi na mimba zitakazofuatia alazimika kujifungua kwa upasuaji pia.

Dhana hii imekita vichwani mwa wanawake wengi, lakini si kweli.

Mwananchi limezungumza na baadhi ya wataalamu wa afya ambao wanasema upo uwezekano wa mama huyo akajifungua kwa njia ya kawaida pia baada ya kufanyiwa upasuaji kwa mtoto wa awali.

Na hiyo inaelezwa kwamba atafanya hivyo iwapo tu atakuwa amekidhi sifa na vigezo vya kiafya vitakavyoruhusu kujifungua kwa njia ya kawaida.

Kwa mujibu wa tovuti ya Pregnancybirth&baby, tafiti mbalimbali zilizowahi kufanyika kuhusu jambo hilo zimeonyesha kufanikiwa kwa asilimia 30 hadi 80.

Pia inaeleza kuwa wajawazito watano hadi saba kati ya 1,000 wanaojifungua kwa njia ya kawaida baada ya upasuaji kwa mtoto aliyepita, ndio huripotiwa kupata changamoto.

Hata hivyo, limetolewa angalizo la kuhakikisha kabla ya kufikia hatua hiyo, mhusika aonane na daktari na mkunga ili kufahamu kama ataweza kuhimili kujifungua kwa njia ya kawaida.

Arapha Sulle, mama wa mtoto mmoja aliyejifungua kwa upasuaji anasema huwa anasikia mtu akianza kujifungua kwa upasuaji, basi watoto wanaofuata atajifungua kwa njia hiyo.

“Hivyo hata nikipata ujauzito tena, itanibidi kujiandaa kimwili na kisaikolojia kuwa nitajifungua kwa upasuaji,” anasema Sulle.

Naye Christina Ngaya, mama wa watoto watatu, mmoja aliyejifungua kwa njia ya upasuaji, anasema anatamani akipata ujauzito mwingine ajifungue kawaida.

Ila Maria Christopher, mama wa watoto wawili, anasema alifanikiwa kujifungua mtoto wake wa pili kwa njia ya kawaida baada ya mtoto wa kwanza kujifungua kwa upasuaji na hakukumbana na changamoto yoyote ile.

“Kwa kuwa nilitamani sana mtoto atakayefuata nijifungue kawaida, hivyo nilifuata ushauri wote niliopewa na daktari na kujiandaa kimwili na kisaikolojia, nashukuru Mungu nilijifungua salama na sasa mtoto wangu amefikisha miaka miwili,” anasema.

Akizungumza na Mwananchi, Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Isaya Mhando anasema mama aliyejifungua kwa njia ya upasuaji anaweza kujifungua kwa njia ya kawaida mtoto anayefuata kama atakuwa amekidhi sifa na vigezo vya kufanya hivyo.

Mhando anavitaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na sababu iliyofanya kufanyiwa upasuaji isiwe endelevu, iwe ilitokea tu katika ujauzito huo wa awali ulilazimisha afanyiwe huo upasuaji.

Ametolea mfano; “labda ujauzito uliopita mama alifanyiwa upasuaji kutokana na mtoto kuwa na uzito mkubwa (Big Baby) na ujauzito unaofuata mtoto akawa na uzito wa kawaida, kama hakuna changamoto nyingine, basi mama huyo anaweza kujifungua kwa njia ya kawaida.”

Anasema kwa mjamzito ambaye changamoto zilizomfanya kufanyiwa upasuaji ni endelevu, hataweza kuruhusiwa kufanya hivyo.

Ametaja kigezo kingine kinachozingatiwa ni mshono wa upasuaji uliopita unatakiwa kuwa umefikisha miaka mitatu na kuendelea na uwe umepona kabisa usioleta shida.

“Siyo mtu amejifungua leo kwa upasuaji, baada ya miezi sita amepata ujauzito eti ajifungue kawaida, hiyo kitaalamu hairuhusiwi kwa sababu anaweza kujiweka katika hatari ya kuchanika mshono uliopita,” anasema daktari huyo.

Pia anasisitiza kuwa ili kumfanya mama na mtoto kuwa salama, ni vyema huduma hiyo ikafanyika katika hospitali kubwa.

“Hospitali ambayo ina vifaa na wataalamu wa kutosha kwa ajili ya kujifungua kwa upasuaji wa dharula pindi changamoto ikijitokeza,” anasema Dk Mhando.

Kwa upande wake, Ofisa Mkunga Msaidizi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Bahi, Anitha Mganga anataja jambo lingine linalozingatiwa ili kuruhusu hilo ni hali ya mtoto aliyeko tumboni kama anaruhusu mama ajifungue kwa njia ya kawaida.

“Kama hadi kufikia hatua ya mwisho kila kitu kipo sawa na kujidhihirishia kama mama ana vigezo na hali ya mtoto inaruhusu, anaweza kujifungua kawaida kwa ujauzito unaofuata,” anasema.

Anaongeza kuwa kitaalamu uamuzi wa kuruhusu mama aliyejifungua kwa njia ya upasuaji kujifungua kawaida hautakiwi kuwa wa kukurupuka, kwa sababu ni mtaalamu wa afya anatakiwa kujiridhisha kwa kina kuwa mhusika amekidhi vigezo vya kufanya hivyo.

“Kutozingatia hilo, kunaweza kumuweka mhusika katika hatari ya kuchanika mshono kipindi anapopata uchungu au wakati wa kujifungua,” anasema Mganga.

Tovuti ya Web MD inaainisha baadhi ya vigezo vinavyoweza kuruhusu mama aliyejifungua kwa upasuaji awali kujifungua kawaida.

Miongoni mwa vigezo hivyo ni pamoja na mhusika binafsi kuwa na utayari na kuridhia kujifungua kwa njia ya kawaida, awe amejifungua kwa upasuaji mara moja na awe alipasuliwa sehemu ya chini.

Pia nyonga za mjamzito zinatakiwa ziwe zenye kujitosheleza kupitisha mtoto, mtoto aliye tumboni awe na uzito usiozidi kilo 3.5, asiwe na changamoto nyingine za kiafya ikiwemo shinikizo la damu, mkao mzuri wa mtoto na sifa nyinginezo zinazoruhusu kujifungua kawaida.

Related Posts