Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa hati ya kumkamata popote alipo, mfanyabiashara maarufu nchini, Pravinchandra Chavda (75) baada ya kuruka dhamana katika kesi ya kutoa taarifa za uongo polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Pia, Mahakama hiyo imetoa hati ya kuwaita wadhamini wa mshtakiwa huyo ili waieleze Mahakama sababu za kushindwa kumpeleka mshtakiwa mahakamani.
Chavda, mkazi wa Upanga, anakabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kutoa taarifa za uongo Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kwa lengo la kujipatia ripoti ya upotevu wa hati za viwanja vitano na kisha kujipatia viwanja hivyo kwa njia ya udanganyifu.
Uamuzi huo umetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya baada ya mshtakiwa kushindwa kufika mahakamani hapo bila taarifa huku wadhamini wake nao wakishindwa kufika mahakamani hapo kueleza alipo mtuhumiwa.
Hakimu Lyamuya alifikia uamuzi huo baada ya upande wa mashtaka kuiomba Mahakama itoa hati ya kumkamata mshtakiwa baada ya kukiuka masharti ya dhamana.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga amedai kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa huku ikisubiria mapitio ya mwenendo wa kesi hiyo, uliowasilishwa Mahakaka Kuu kwa ajili ya kupitiwa na kutolewa uamuzi.
“Kesi hii iliitwa kwa ajili ya kutajwa lakini mshtakiwa sijamuona mahakamani hapa wala wadhamini wake na sina taarifa zao, hivyo naiomba Mahakama itoe hati ya kumkamata,” amedai Mwanga.
Pia, ameiomba Mahakama itoe hati ya kuwaita wadhamini wake ili wafike mahakamani kueleza kwanini wameshindwa kumpeleka mshtakiwa huyo mahakamani.
Hakimu Lyamuya amekubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kutoa hati ya kukamatwa kwa mshtakiwa na wito kwa wadhamini, kisha, amwahirisha kesi hiyo hadi Desemba 17, 2024 itakapotajwa.
Mshtakiwa anadaiwa Januari 10, 2022 jijini Dar es Salaam alijipatia kiwanja namba 1814 kilichopo Msasani Peninsula jijini Dar es Salaam kwa njia ya udanganyifu baada ya kuwasilisha kwa Msajili wa Hati, nyaraka ya uhamisho wa kiwanja hicho akijifanya yeye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Sole, kampuni ya uwekezaji inayomiliki kiwanja hicho wakati akijua sio kweli.
Oktoba 7, 2019 katika Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Chavda anadaiwa kutoa taarifa za uongo kuhusiana na upotevu wa hati tano za viwanja, kwa lengo la kujipatia hati za upotevu wa mali hizo wakati akijua si kweli.
Pia inadaiwa mshtakiwa huyo akiwa jijini Dar es Salaam, alighushi nyaraka inayoitwa Maazimio ya Bodi, akijaribu kuonyesha kwamba nyaraka hiyo ni halisi na imetolewa na Mkurugenzi wa Point Investment Limited, mmiliki wa kiwanja hicho, wakati akijua si kweli.
Pia, anadaiwa Januari 10, 2022, katika Jiji la Dar es Salaam, aliwasilisha nyaraka hiyo ya kugushi kwa Msajili wa Hati, akionyesha kwamba aliuziwa kiwanja namba 1814 kilichopo Msasani Peninsula.