TMA yatoa angalizo la mvua kubwa

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ikieleza kuhusu matarajio ya hali mbaya ya hewa kwa siku tano katika maeneo machache ya ukanda wa Ziwa Victoria na Magharibi ya nchi.

Taarifa ya TMA iliyotolewa Alhamisi Novemba 21, 2024 inatoa angalizo la mvua kubwa kwa maeneo machache ya ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu) na maeneo ya Magharibi ya nchi (Mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi).

Kwa mujibu wa TMA, uwezekano wa uwepo wa mvua hizo ni wa wastani, ikieleza kiwango cha athari zinazoweza kutokea kuwa cha wastani.

Athari zinazoweza kujitokeza kwa mujibu wa TMA ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, ikiwataka wananchi kuzingatia taarifa hiyo na kujiandaa.

TMA imeeleza angalizo hilo ni kati ya Alhamisi hadi Jumamosi Novemba 23, 2024.

Mbali na taarifa hiyo, TMA ilishatoa mwongozo kwa sekta za usafirishaji, mamlaka za miji na menejimenti ya maafa kuchukua tahadhari ya mvua za msimu wa Vuli.

Sekta nyingine zilizotakiwa kuchukua tahadhari ni za kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, afya na sekta binafsi.

Tahadhari hiyo ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Ladislaus Chang’a Oktoba 31, 2024 katika mkutano na waandishi wa habari akieleza kuhusu mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka.

Maeneo hayo ni ya kanda za Magharibi, Kati, Nyanda za Juu Kusini Magharibi, Kusini mwa nchi, Ukanda wa Pwani ya Kusini na yaliyopo Kusini mwa Mkoa wa Morogoro.

Alisema maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Singida na Dodoma; kaskazini na mashariki mwa Mkoa wa Lindi na kaskazini mwa mikoa ya Mbeya na Iringa yatakuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani.

Alisema mikoa ya Njombe, Ruvuma, Mtwara, maeneo ya kusini na magharibi mwa Mkoa wa Lindi, kusini mwa mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro yatapata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Alisema mvua zilitarajiwa kuanza wiki ya nne ya Oktoba katika Mkoa wa Kigoma na ifikapo Novemba itasambaa maeneo mengine yanayopata mvua za msimu, huku Mkoa wa Ruvuma zikitarajiwa kuanza Desemba.

Alisema kipindi cha nusu ya pili ya msimu kati ya Februari hadi Aprili, 2025 kitakuwa na mvua nyingi ikilinganishwa na nusu ya kwanza ya Novemba, 2024 hadi Januari, 2025.

Related Posts