Kwa mujibu wa uzoefu wetu, tumeshuhudia au kusikia kuhusu visa vinavyosababisha migogoro, kuvunjika au kudorora kwa ndoa.
Na miongoni mwa sababu kubwa zinazotajwa ni pamoja na kiburi cha “usomi.” Inaelezwa kuwa hiyo ni sumu mbaya sana kwenye maisha ya ndoa.
Tuanze na hadithi. Kulikuwa na mwanamume mmoja ambaye elimu yake aliishia darasa la nne, lakini kwa juhudi zake aliweza kufanikiwa kimaisha na kupata utajiri.
Alipoamua kuoa, alimuoa mwanamke aliyemaliza kidato cha nne, ingawa alifeli mitihani yake ya mwisho.
Kwa sababu ya elimu hiyo ndogo, mwanamke huyo alijiona yeye ndiye msomi zaidi kuliko mumewe, japokuwa hakuwa na mafanikio makubwa kama yake.
Sasa kutokana na mfano huo, najiuliza hivi wako wangapi wenye tabia kama ya huyu? Yaani elimu ya kidato cha nne inakufanya ujione bora! Najiuliza tena, je, ukiwa na elimu ya PhD itakuwaje?
Licha ya kutoka katika familia maskini na kukosa sifa za juu za kuolewa, mwanamke huyu alijiona msomi wa kupigiwa mfano, wakati ukweli ni kwamba, dhana ya usomi ni zaidi ya shahada. Usomi sio kuingia darasani tu, bali ni kuwa mnyenyekevu, mwenye busara na mwenye utayari wa kusaidia wengine.
Usomi ni kama kipofu anayemwona aliyefumbuliwa macho na unajumuisha kujua udhaifu wako na kutambua nguvu za wengine hata kama unawazidi kwa elimu.
Ndoa haina “shahada.” Maisha ya ndoa yanahitaji unyenyekevu na ufahamu wa thamani yako na ya mwenzi wako.
Hivyo, hata kama una elimu zaidi ya mwenzi wako, usomi wako haupaswi kuwa kibali cha kumdhalilisha, kumkandamiza au kumchukia. Usomi si majivuno, bali ni kujua nafasi yako na kuitumia kwa upole.
Kurudi kwenye hadithi yetu, mwanamke huyu alijiona bora kwa sababu tu alifikia elimu ya kidato cha nne na kwa kujiamini huku, kukamfanya akose heshima kwa mumewe. Usomi unapaswa kukufanya uwe na heshima na upendo kwa wengine.
Kutokana na ujinga na kiburi, mwanamke huyu alikosa heshima kwa mumewe na badala yake alijikita katika mambo yasiyofaa.
Sasa kama kweli elimu ilikuwa muhimu kwake, kwa nini hakusema mapema kabla ya ndoa? Jawabu ni rahisi; alifuata utajiri wa mumewe huku akijiona msomi kwa upumbavu wake. Hivyo, iwe mwanamke au mwanamume, hakuna anayepaswa kutumia elimu, utajiri, au chochote kumdhalilisha mwenzake.
Kabla ya kumuumiza, kumkosea heshima au kumdhalilisha mwenzako, jiulize, “Je, wazazi wangu na jamaa zangu walikuwa na elimu gani?”
Hata kama walikuwa wasomi, hiyo haitoi kibali cha kumdhalilisha mwenzio. Jiweke kwenye nafasi ya mwenzako na jiulize, “Ningetaka kutendewa vipi kama ni mimi?”
Kama kweli ulimhitaji msomi au tajiri, kwa nini hukuchagua wasomi au watu wenye mali kubwa?
Ni wazi kuwa wanaotoa visingizio vya aina hii ni matapeli wa ndoa wanaotumia nafasi ya ndoa kujinufaisha.
Tunashauri wale wenye tabia hizi za kiburi wabadilike na waathirika wa tabia hizi wasimame kidete na kuuliza maswali magumu. Hata kama ungekuwa umesoma, kumbuka kuwa usomi si kiburi, bali ni unyenyekevu, msaada kwa wengine sambamba na heshima.
Imeandikwa na Nesaa na Nkwazi Mhango