Mwanza. Serikali kupitia Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico), imeanza mchakato wa kujenga meli ya mizigo katika Bahari ya Hindi ikiwa ni mkakati wa kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwenda mashariki ya mbali.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa jina na nembo mpya ya kampuni hiyo iliyobadilishwa kutoka iliyokuwa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) na kuwa Tashico, Mkurugenzi Mtendaji wake, Eric Hamissi amesema hadi kufikia mwaka 2030, meli nne zitakuwa zimejengwa katika Bahari ya Hindi.
“Mchakato umeanza wa kuwa na meli zetu Bahari ya Hindi, mwaka huu tunamalizia upembuzi yakinifu na mwaka kesho tunaanza na ujenzi wa meli moja ya mzigo,” amesema Eric.
Amesema mchakato wa kubadili jina umeanza tangu mwaka 2021 ukihusisha wataalamu kutoka ndani ya taasisi za Wizara ya Uchukuzi, Ofisi ya Hazina na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ukiwa na lengo la kuboresha taswira ya umiliki, kufika mashariki ya mbali kwa upande wa usafirishaji majini na pia kujiimarisha kibiashara.
“Sasa kampuni ina idadi ya meli 18 na boti moja ya kitalii…kati ya meli hizo, zinazofanya kazi ni nane,” amesema Eric wakati akielezea historia ya kampuni hiyo iliyofufuliwa na Serikali mwaka 2019/20, baada ya kushindwa kujiendesha.
Ameongeza kuwa “Uwekezaji wa kwanza ulianza 2019/20, ulihusisha urekebishaji wa meli ya Mv Victoria, Mv Butiama, ujenzi wa meli mpya ya Mv Mwanza na cherezo. Kampuni imefanikiwa kurejesha meli tatu zilizokuwa zimesimama na kuchakaa kabisa na kuongeza meli tatu mpya katika Ziwa Nyansa.”
Akizindua jina na nembo ya kampuni hiyo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ameiagiza menejimenti ya Tashico kuongeza ubunifu wa huduma kwa wateja, kuwasimamia wakandarasi wanaotekeleza ujenzi na ukarabati wa meli za shirika na kuimarisha usimamizi wa mapato ili kuliepusha shirika kupata hati chafu.
Pia, ameiagiza menejimenti hiyo kuweka mkakati unaotekelezeka wa kupata wataalamu katika maeneo mbalimbali, hususan makapteni na wahandisi wa meli, ili kutotegemea wataalamu kutoka nje ya nchi.
Amesema matarajio yake ni kuiona Tashico ikianza kutoa gawio kwa Serikali kupitia faida wanayoipata.
“Ninatambua kuwa pamoja na mipango inayotekelezwa kwa sasa ya ujenzi wa meli katika maziwa yetu, mpango wa muda mrefu ni kujenga meli katika Bahari Kuu. Hii ni hatua kubwa sana ambayo itaifanya kampuni yetu kuwa na ushindani mkubwa katika soko la ndani na nje ya mipaka yetu,” amesema Kihenzile.
Ameipongeza kampuni hiyo kwa kuongeza mapato yake kutoka Sh1 bilioni mwaka 2019 hadi Sh8 bilioni mwaka 2024.
Mwenyekiti wa Bodi ya Tashico, Meja Jenerali Mstaafu, John Mbungo ameahidi kusimamia shughuli za kampuni hiyo kwa weledi ili kuhakikisha uwekezaji wa Serikali ambao ni zaidi ya Sh1 trioni unakuwa na tija kwa umma, ikiwemo kuongeza ukusanyaji wa mapato kupitia huduma.
“Meli zetu sasa zinaendana na jina letu la Tashico ambalo linaashiria kampuni ya kitaifa inayojishughulisha na usafirishaji kwa njia ya maji, hii inatupa fursa ya kutanua wigo na kuitangaza nchi yetu. Ninatoa ahadi ya kuendelea kusimamia shirika hili kwa weledi,” amesema Mbungo.