Mbowe na wenzake washikiliwa Polisi Songwe

Songwe. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo  (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Songwe kwa mahojiano baada ya kile kinachoelezwa kukiuka utaratibu wa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa.

Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 22 Kamanda wa Polisi mkoani Songwe, Augustino Senga amethibitisha kumshikilia kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani nchini pamoja na watu wengine.

“Ni kweli tunaashikilia Mbowe na viongozi  wengine japo idadi yao bado sijaipata, kwa mahojiano zaidi kutokana na kukiuka utaratibu wa kampeni.

“Aliposhuka uwanja wa ndege alipopokelewa kusalimia akataka kuweka na mkutano hapohapo, jambo ambalo si sahihi kwa kuwa vyama vyote viliwasilisha maeneo ya mikutano yao,” amesema kamanda huyo.

Jeshi la Polisi likidaiwa kuwatawanya wananchi eneo la Mlowo, Songwe waliofika kumskiliza Mwenyekiti wa Chama Taifa Mhe Freeman Mbowe.

Ametoa rai kwa vyama vyote kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za uchaguzi akieleza kuwa jeshi hilo halitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayeenda kinyume, hasa kipindi hiki.

Kauli hiyo imetolewa baada ya taarifa kusambaa kwenye mitando ya kijamii, ikizungumzia tukio la kukamatwa kwa Mbowe.

Mkurugenzi wa mambo ya Nje na Mawasiliano wa Chadema, John Mrema ameandika kwenye ukurasa wake wa X: “Jeshi la Polisi limevamia msafara wa Mwenyekiti wa Chama Taifa Mheshimiwa Freeman Mbowe akiwa njiani kuelekea Vwawa, Wilaya ya Mbozi kwenye uzinduzi wa kampeni Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mchana huu.”

Related Posts