Wikiendi ya turufu muhimu Ligi Kuu Bara

HAKUNA zaidi ya hesabu wikiendi hii kwenye Ligi Kuu Bara. Zinapigwa mechi tatu muhimu kwenye Ligi Kuu Bara ingawa kwa namna yoyote haziwezi kumchomoa aliyeko kileleni.

Lakini ni turufu muhimu kwenye mbio za kumi la pili. Azam FC inahitaji ushindi wowote dhidi ya Kagera Sugar ili kumshusha Yanga nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi. 

Azam ambayo ipo nafasi ya nne kwenye msimamo baada ya kukusanya pointi 21 imefunga mabao 13 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara tatu ikishinda itafikisha pointi 24 na kuishusha Singida Black Stars (23) na Yanga (24) utofauti utakuwa kwenye mabao ya kufungwa na kufunga.

Azam dhidi ya Kagera Sugar rekodi zinambeba mwenyeji wa mchezo huo kutokana na kushinda kwenye mechi tano za mwisho timu hizo kukutana ameshinda tatu sare moja na ushindi mmoja kwa Kagera.

Kocha mkuu wa Kagera Sugar, Melis Medo alisema; “Tunahitaji kuendeleza ubora kwenye mchezo huu baada ya kupata matokeo mchezo wetu wa mwisho dhidi ya Dodoma Jiji haitakuwa rahisi lakini tumejiandaa kyuonyesha ushindani kwa wapinzani wetu lengo ni kuona tunakuwa na mwendelezo mzuri.”

Kocha wa Azam FC, Rachid Taoussi alisema;”Natarajia mchezo mzuri na wa ushindani dhidi ya Kagera Sugar mipango yangu ni kukusanya pointi tatu ili kuendelea kusogea nafasi za juu kwenye msimamo na hatimaye kutwaa taji la ligi msimu huu.”

MBEYA; Mchana wa jua kali, Jijini Mbeya Ken Gold iliyofunga mabao manne kwenye mechi zao tano zilizopita itaikaribisha Coastal Union mchezo unaopigwa kwenye uwanja wa Sokoine.

Kwenye mchezo huo mwenyeji Ken Gold ataingia kwenye mchezo huo akiwa na kumbukumbu ya kutoka kupoteza dhidi ya Tanzania Prisons huku Coastal Union itaingia ikiwa na kumbukumbu ya kutoka kuambulia suluhu dhidi ya Singida Black Stars.

Kitakwimu msimu huu, KenGold imeambulia pointi tano katika mechi zao tano za nyumbani. Huku Coastal wakipata pointi tatu ugenini.

KIGOMA; Mchezo mwingine utapigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika saa 10:15 jioni Mashujaa ambayo imetoka kupoteza mechi tatu mfululizo itakuwa nyumbani itaikaribisha Namungo iliyotoka kuchapwa bao 1-0 KMC mechi ya mwisho.

Mpaka sasa Mashujaa ina pointi nane kwenye mechi sita za nyumbani, huku Namungo ikipata pointi tatu tu ugenini katika mechi tano.

Kocha wa Mashujaa, Mohamed Abdallah ‘Bares’ alisema; “Tutaingia kwa kuwaheshimu wapinzani wetu Namungo ni timu nzuri ipo chini ya kocha mwenye uzoefu naamini mbinu bora ndio zitakazoamua matokeo.”

Juma Mgunda kocha wa Namungo alisema hautakuwa mchezo rahisi wanakutana na timu ambayo ipo timamu inacheza kwa kutumia nguvu hivyo wamejiandaa vyema kwenda kukabiliana nayo.

Related Posts