Bunda. Watu wanne wamefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa huku mmoja akiwa katika hali mbaya, baada ya lori lililokuwa limepakia mawe kuacha njia na kuwagonga wafanyabiashara pamoja na jengo moja.
Ajali hiyo imetokea leo Ijumaa Novemba 22, 2024 saa 5:40 asubuhi katika makutano ya barabara ya Mwanza – Bunda na Nyamuswa – Ukerewe mjini Bunda ambapo waliofariki ni wanaume watatu na mwanamke mmoja.
Waliofariki katika ajali hiyo ni Nyahiti Simon (32), Hekima Jackson (25), Nuru Abdul (40) na Alphonce Dengu (45), wote wakazi wa mjini Bunda.
Majeruhi katika ajali hiyo ni pamoja na Baraka Bahati (19), Philipo Yusufu (36), Juma Maenzeka (23), Issa Mwita (31), Juma Nyagina (40) na John Ncheye (40), wote wakiwa ni wakazi wa mjini Bunda.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amethibisha kutokea kwa ajali hiyo, huku akisema taarifa za awali zinaonyesha gari hilo lilifeli breki na kisha kuparamia wafanyabiashara pamoja na jengo moja lililokuwa na maduka.
“Gari lililokuwa linatokea barabara ya Nyamuswa kuelekea Ukerewe, liliparamia jengo hilo ambalo pia pembeni yake kuna gereji na kusababisha vifo vya watu wanne na majeruhi saba. Tumefanikiwa kufika eneo la tukio mapema na kuwatoa waliohusika kwenye ajali na kuwawahisha majeruhi hospitalini kwa ajili ya matibabu,” amesema.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Dk Yusufu Wambura amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda.
Amesema vifo vya watu hao vimetokana na kukandamizwa na mawe pamoja na ukuta ambao ulibomoka wakati wa ajali hiyo.
Amesema kufuatia ajali hiyo, majeruhi wanne wamelazwa katika hospitali hiyo huku wengine wawili wakitibiwa na kuruhusiwa baada ya hali zao kuwa nzuri na mmoja kupewa rufaa kwenda katika hospitali ya Kanda ya Bugando kwa matibabu zaidi.
“Huyu wa Bugando amevunjika mbavu pande zote mbili, tukaona anahitaji huduma za juu na kwa haraka na hivi tunavyoongea hapa, tayari amepokelewa Bugando,” amesema
Akizungumzia hali za majeruhi waliolazwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda, Dk Wambura amesema wamelazimika kumkata mguu majeruhi mmoja ambaye alifikishwa hospitalini hapo mguu ukiwa umeharibika
Amesema majeruhi mwingine pia ameonyesha dalili za kupasuka bandama, hivyo wamelazimika kumpeleka kwenye chumba cha upasuaji kwa ajili upasuaji, huku wengine wawili hali zao zikiwa zinaendelea vizuri.
Mmoja wa mejeruhi hao, Baraka Bahati ambaye ni fundi gereji, amesema akiwa anaendelea na shughuli zake, ghafla alimuona mzee mmoja akikimbia na alipogeuka kuangalia kilichokuwa kinaendelea ghafla gari likawa limefika.
“Kwa ujumla hata sijui nini kimetokea maana nilipogeuka tu nikawa nimefikiwa na nimekuja kushtuka niko hapa hospitalini,” amesema.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamesema walishuhudia gari likiwa limepoteza mwelekeo na kupaa kabla ya kutua kwenye jengo lililokuwa na vibanda vya maduka.
Samuel Mng’onya amesema baada ya ajali kutokea, walifika katika eneo hilo kwa ajili ya kutoa msaada ambapo miongoni mwa waliofariki ni pamoja na dereva wa gari hilo ambaye alifia hapo hapo baada ya kubanwa.
“Wengi waliofariki walibanwa kwa sababu gari lilikuwa na mawe, sasa likawa limegonga ukuta ambao pia ulibomoka na ndani kulikuwa na vitu, kwa hiyo wakajikuta hawana namna ya kutoka, hawa majeruhi wengi wao walikuwa kwa pembeni kidogo ingawa kuna mmoja ambaye naye alifunikwa na mawe lakini ametolewa akiwa hai japokuwa hali yake haikuwa nzuri,” amesema Sylivester John.
Shuhuda mwingine, Chacha Meremo ametoa wito kwa Jeshi kwa Polisi na mamlaka husika kuhakikisha kuwa wanafanya ukaguzi wa magari hasa yanayobeba mawe na mchanga ili kuhakikisha hayana dosari.
“Kwa nilivyoona pale, inaonekana shida ilikuwa ni breki, kama ukaguzi ungekuwa unafanyika, polisi wangegundua mapema na gari lisingeruhusiwa kuingia barabarani,” amesema Meremo.