Refa msaidizi wa kimataifa wa Tanzania, Mohammed Mkono ni miongoni mwa waamuzi wanne wa Tanzania walioteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) kuchezesha mechi ya kuwania kufuzu fainali za Chan 2024 kati ya Uganda na Burundi itakayochezwa jijini Kampala, Uganda, Jumatano ijayo, Novemba 27.
Mechi hiyo ambayo itakuwa ya kwanza ya raundi ya pili ya mashindano hayo itachezwa katika Uwanja wa Nelson Mandela kuanzia saa 10:00 jioni.
Mkono ambaye msimu uliopita aliibuka mshindi wa tuzo ya refa bora msaidizi, ameteuliwa kuwa mwamuzi msaidizi namba moja na atachezesha mechi hiyo na Watanzania wenzake, Nasir Siyah ambaye atakuwa mwamuzi wa kati, Hamdani Said ambaye atakuwa refa msaidizi namba mbili na Elly Sasii atakayekuwa refa wa akiba.
Solomon Gebresillasie kutoka Ethiopia ameteuliwa kuwa kamishina wa mechi hiyo na mtathmini wa marefa atakuwa ni Sanusie Rashid kutoka Sierra Leone.
Uteuzi wa Mkono na wenzake umekuja wiki moja tangu marefa Ahmed Arajiga, Frank Komba, Hamdani Said na Sasii walipochezesha mechi ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 baina ya Lesotho na Afrika ya Kati ambao Lesothi iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Mwezi uliopita, Mkono alikuwa refa msaidizi namba moja katika mechi ya kuwania kufuzu Afcon ambayo Guinea Ikweta iliibuka na ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Liberia.
Katika mchezo huo ambao ulifanyika katika Uwanja wa Taifa wa Malabo, Guinea Ikweta, refa wa kati alikuwa ni Arajiga, Kassim Mpanga akiwa refa msaidizi namba mbili na refa wa akiba alikuwa ni Ramadhan Kayoko.