Moshi. Makandarasi wa miradi iliyotekelezwa chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) mkoani Kilimanjaro, wamesema wanahofia kufilisiwa na taasisi za fedha kutokana na kutolipwa malipo ya kazi tangu Mei 2024.
Wakizungumza na Mwananchi, jana, baadhi ya wakandarasi walisema wengi wao wana madai ya muda mrefu na kwamba Mkoa wa Kilimanjaro unaoongoza kwa kiwango cha madai ambayo ni karibu Sh10 bilioni hadi kufikia Mei kulinganisha na mikoa mingine.
Kufuatia malalamiko hayo, Meneja wa Tarura Mkoa wa Kilimanjaro, Nicholous Francis amesema leo Novemba 22, 2024 kuwa tayari malalamiko ya makandarasi hao wameshaanza kuyafanyiwa kazi na baadhi yao wameshaanza kulipwa.
“Tuliingia mkataba na baadhi ya makandarasi na sasa wanaendelea kulipwa kadri ambavyo tunazidi kupata fedha,” amesema.
“Karibu kila baada ya siku sita, wiki huwa tunawalipa lakini hatulipi wote, tunawalipa wale ambao tayari ‘certificate’ zao zilishatangulia, ndio tunawalipa,” amesisitiza meneja huyo wa Tarura.
Kuhusu idadi ya wakandarasi wanaodai fedha zao na kiasi wanachodai, amesema yupo nje kikazi na hakuwa na takwimu na kiasi cha fedha wanazodai.
Hata makandarasi hao wamesema ingawa hawana takwimu halisi, lakini madai ya wakandarasi ni makubwa kutokana na miradi ya barabara, vivuko na madaraja waliyoitekeleza na kuikamilisha kwa ufanisi hadi Mei.
“Kazi zimesimama nyingi na baadhi ya miradi makandarasi wameondoka eneo la mradi. Dhamana tulizoweka benki kupata mikopo zipo hatarini kuuzwa. Binafsi nyumba yangu iko hatarini kuuzwa,” alidai mmoja wao.
Mkandarasi mwingine ambaye pia aliomba jina lake lisitajwe, ameiomba Serikali kuona namna ya kuongea na benki zinazowadai, ili wasitishe kutoza riba hadi pale watakapolipwa.
“Unajua unapokopa unakuwa umejipanga kuwa huu mradi nitakuwa nimemaliza ndani ya muda fulani. Sasa unamaliza mradi unakaa zaidi ya miezi sita hulipwi na hakuna maelezo yanayoeleweka. Serikali itusaidie katika hili,” alieleza.
Mwenyekiti wa makandarasi hao, Eliukunda Msaki alithibitisha uwepo wa makandarasi wanaoidai Tarura kwa muda mrefu akisisitiza hali ni tete.
“Ni kweli kabisa wakandarasi wengi tumemaliza kazi tulizosainishwa mikataba kuwa hela zipo, wengi tumeingia benki tumechukua mikopo ili kupata mitaji ya kutekeleza ile miradi, tumemaliza miradi lakini hatulipwi,” alisema Msacky.
“Waajiri wetu kwa maana ya Tarura wanasema hela hakuna, hawajatumiwa hela. Sasa hicho kitu kinaumiza watu wengi, mimi mwenyewe na watu wengi tu,” alisema.
“Hapa tulikuwa tunaumiza vichwa tufanye nini, tuchukue hatua gani au tupaze sauti ya aina gani. Tulikuwa tunafikiria kuitisha kikao (cha wakandarasi) tumwite meneja wetu wa kanda na mkoa ili tupaze sauti zetu,” amesisitiza.
Agosti 30, 2024, suala la madeni ya wakandarasi lilitinga bungeni ambapo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alilitolea ufafanuzi na kuwa Serikali imeendelea kulipa malipo hayo na mengine ni ya muda mrefu.
“Si kwamba serikali imeacha kulipa bali kinachojitokeza ni kwamba kumekuwepo na malimbikizo ya madeni ya muda mrefu,” alieleza Waziri wa Fedha katika maelezo yake.
Dk Nchemba alisema pamoja na uwepo wa malimbikizo ya muda mrefu, Serikali imejitahidi kulipa madeni hayo na hadi kufikia mwaka huu, madeni ya wakandarasi yalikuwa chini ya Sh400 bilioni.