BEKI wa zamani wa Dodoma Jiji, Amani Kyata ameungana na aliyekuwa kocha wake Melis Medo kuunda benchi la ufundi la Kagera Sugar.
Kyata ambaye alikuwa akiitumikia Mtibwa Sugar aliyojiunga nayo Agosti 2024, ameachana na timu hiyo baada ya kuumia goti ambalo lilimuweka nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi miwili.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kyata alisema aliamua kuingia kwenye kozi ya ukocha baada ya kuwa nje ya uwanja akijiuguza jeraha la goti na sasa amepata leseni C.
“Nimesomea ukocha lakini bado sijapata sifa ya kuwa kocha msaidizi licha ya kupata nafasi hiyo hapa Kagera Sugar naifanya kwa muda huku nikiwa naendelea kupata elimu zaidi,” alisema na kuongeza.
“Mbali na taaluma hiyo pia natumika kuwasoma wapinzani na uchambuzi wa video na nina taaluma nayo kwani nilisomea wakati bado nacheza mpira.”
Mbali na hivyo, Kyata amebainisha ana elimu ya ukocha wa viungo na utimamu wa mwili kutokana na mafunzo aliyoyapata kutoka Major Sports Institute chini ya mkufunzi Nyasha Charandura ambaye ni mtaalamu wa sayansi ya michezo wa Taifa Stars pamoja na Azam.
Bado Kagera Sugar hawajaweka wazi nafasi ya Kyata katika benchi lao la ufundi lakini alikuwepo wakati timu hiyo ilipocheza dhidi ya Pamba Jiji Oktoba 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.
Mchezo huo ndio ulikuwa wa kwanza kwa Melis Medo tangu akabidhiwe kikosi hicho baada ya kuondolewa kwa Paul Nkata.
Kyata amezitumikia timu kadhaa zikiwemo za nchini Kenya ambazo ni Chemelil Sugar (Kenya), Nakumatt (Kenya), Mount Kenya United (Kenya) na Kariobangi Sharks (Kenya), huku zile za Tanzania zikiwa ni African Lyon, Mwadui, Namungo na JKT Tanzania.
Pia amecheza Coastal Union, Dodoma Jiji na Mtibwa Sugar na huko kote amefundisha na Melis Medo.