Songwe. Watu watano wamefariki dunia mkoani Songwe baada ya kutokea ajali iliyohusisha lori aina ya Scania na bajaji.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Songwe, Augustino Senga amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, jana, Ijumaa Novemba 22, 2024 saa 3:15 usiku, ambapo bajaji ilikuwa ikitokea barabara ya mji mdogo wa Mpemba ikielekea Tunduma.
Kwa mujibu wa Kamanda Senga, waliofariki dunia ni Emmanuel Kalinga (dereva wa bajaji), Rehema Sikamnga (25), Festo Aron Mambwe (57), Rosemary Njema (44) na Milembe Siyantemi (36).
Amesema ajali hiyo ilitokea baada ya bajaji hiyo yenye namba MC783 DUF, aina ya TVS, kujaribu kuyapita magari mengine yaliyokuwa mbele yake kisha kugongana na gari lenye namba za usajili T958 BCS aina ya Scania.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Kituo cha Afya cha Tunduma kilichopo Wilaya ya Momba na chanzo cha ajali hiyo bado kinachunguzwa, huku dereva wa Scania akiwa anatafutwa.
“Jeshi la Polisi Mkoa Songwe linatoa wito kwa madereva na wamiliki wa vyombo vya moto kukagua vyombo vyao kabla ya kuanza safari na kuzingatia sheria za usalama barabarani wakati wote,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.