Minziro: mambo yatakaa sawa | Mwanaspoti

LICHA ya kufungwa bao 1-0 na Simba juzi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Kocha wa Pamba Jiji, Fredy Felix ‘Minziro amesema kwa soka walilocheza vijana wake na ushindani walioonyesha, anaamini sasa wameiva na wako fiti kwa ajili ya kuanza kupata matokeo mazuri katika mechi za Ligi Kuu Bara.

Huo ulikuwa mchezo wa tano mfululizo nyumbani kwa Pamba Jiji bila ushindi tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Minziro aliyetua klabuni hapo Oktoba 17, mwaka huu akirithi mikoba ya Goran Kopunovic, juzi ulikuwa mchezo wake wa tano kuiongoza timu hiyo huku akishinda mmoja, sare mmoja na kupoteza mitatu.

Akizungumzia mchezo wa juzi, Minziro alisema kwa alichokiona dhidi ya Simba namna wachezaji wake walivyopambana na kutimiza aliyoelekeza basi muda siyo mrefu ataanza kuvuna matunda ya falsafa mpya alizoingiza kwenye timu hiyo tangu atue hapo.

“Naamini wachezaji wangu wameshakuwa fiti na mimi ni muumini wa soka la kushambulia, kwa hiyo nategemea hizi mechi zinazokuja tunakwenda kushambulia kutafuta mabao na lazima yatapatikana, watu wa Pamba na Mwanza kwa ujumla waisapoti timu mwisho wa siku tutoke huku chini,” alisema Minziro.

Kocha huyo aliipongeza Simba huku akiamini ubora wa wachezaji wake ndiyo uliamua matokeo hayo licha ya vijana wake kupambana lakini tukio la penalti ya mapema liliathiri saikolojia ya wachezaji wake.

Related Posts