KenGold yawang’ang’ania Wagosi Sokoine | Mwanaspoti

Bao la kusawazisha dakika ya 90 limeiokoa Ken Gold kupoteza mchezo nyumbani dhidi ya Coastal Union na kufanikiwa kubaki na pointi moja katika Uwanja wa Sokoine jijini hapa.

Sare hiyo inakuwa ya tatu kwa timu hiyo baada ya kufanya hivyo dhidi ya Dodoma Jiji 2-2 na Tabora United 1-1 huku ikiendelea kubaki mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa pointi sita ikicheza mechi 12.

Katika mchezo wa leo, Coastal Union walitangulia kupata bao dakika ya 45 kupitia Abdalah Hassan.

Kipindi cha pili Ken Gold walionesha utulivu wakilisakama sana lango la ‘Wagosi wa Kaya’ lakini mashambulizi yao yalidhibitiwa vyema na mabeki wa upinzani.

Hata hivyo, dakika ya 90 Emanuel Mpuka aliisawazishia  Ken Gold na kurejesha matumaini na ari kwa wenzake licha ya mtihani mzito walionao hadi sasa katika vita ya kujinasua kushuka daraja.

Huu unakuwa mchezo wa nne kwa Kocha mpya wa Coastal Union, Juma Mwambusi akishinda mmoja dhidi ya Kagera Sugar na sare mbili dhidi ya Singida Black Stars 0-0 na Ken Gold 1-1 huku akipoteza mbele ya Yanga bao 1-0.

Straika wa Coastal Union, Maabad Maulid amesema kupata pointi moja ugenini si matokeo mabaya akieleza kuwa kwa sasa ligi ni ngumu hakuna timu nyepesi kuruhusu kufungwa.

Kuhusu kasi ya ufungaji, nyota huyo Mzanzibar amekiri vita kuwa ngumu akieleza kuwa mabeki wamekuwa makini kuharibu mipango yake akifafanua kuwa anashukuru matokeo ya timu si mabaya sana.

“Msimu huu tumeuanza kiugumu, hakuna timu nyepesi lakini hata mabeki wamekuwa wagumu kutoruhusu mashambulizi, bado ni mapema na lolote linaweza kutokea huko mbele, kikubwa ni kupambana kila mechi.

“Kujituma na nidhamu ya ndani na nje ndio sababu kubwa ya kuaminiwa na makocha wanaokuja, wananiamini wakielewa naweza kusaidia timu na matarajio yetu ni kufanya vizuri,” amesema straika huyo.

Related Posts