Kocha wa makipa wa Tabora United, Khalfan Mbonde, amesema maandalizi yao kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida Black Stars utakaochezwa kesho Novemba 24, 2024 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora yamekamilika lakini wana hofu ya kukamiwa na wapinzani wao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mbonde amesema baada ya timu hiyo kuifunga Yanga, wanaamini hivi sasa kila timu itawakamia watakapocheza nayo.
“Tunaamini kwamba kesho tutakutana na mchezo mgumu dhidi ya Singida Black Stars lakini tumejipanga kuendeleza ushindi kwenye michezo yetu japokuwa tunaamini kwamba baada ya kuifumga Yanga kila timu itatukamia kila tutakapocheza lakini tumejipanga kuhakikisha matokeo mazuri yanapatikana kwenye kila mchezo tutakaocheza,” alisema Mbonde na kuongeza:
“Tumekaa siku 10 bila kucheza mechi ya ushindani, tumepata muda wa kukiandaa kikosi chetu kwa kucheza michezo ya wenyewe kwa wenyewe na makosa binafsi tumeyarekebisha kwa kiwango kikubwa, hivyo mchezo wetu na Singida tunaamini tutapata matokeo mazuri.”
Hata hivyo, Mbonde amesema kuelekea mchezo huo watawakosa wachezaji wawili ambao ni Salum Chuku na Matthew Odongo awali walikuwa Singida Black Stars ambapo kwa mujibu wa mikataba yao timu hizo zinapokutana hawataruhusiwa kucheza.
Kocha Msaidizi wa Singida Black Stars, Denis Kitambi, amesema kuelekea mchezo huo wamejiandaa vyema huku wakitarajia kumkosa kiungo mshambuliaji, Marouf Tchakei ambaye ameumia bega.
“Maandalizi yetu yako kamili kwani tumekuja na wachezaji ambao tunaamini watatusaidia kwenye mchezo huu kupata matokeo mazuri, tunaamini mpinzani wetu ataingia kwenye huo mchezo kwa kujiamini baada ya kupata matokeo mazuri dhidi ya Yanga lakini sisi tumekuja na mpango wetu wa kuhakikisha tunafanya vizuri.
“Kwa michezo miwili iliyopita tulikuwa na changamoto ya kushindwa kufunga mabao licha ya kupata nafasi nyingi lakini kwa muda wa mapumziko uliopita tumefanyia kazi mapungufu yote hivyo mashabiki wajitokeze kuutazama mchezo huu kwani utakuwa maalumu kwa upande wetu kurejesha ari ya ushindi baada ya kutofanya hivyo kwa dakika 180 zilizopita,” alisema Kitambi.
Mpaka sasa Singida Black Stars ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya michezo 10 ambapo imekusanya alama 23 huku Tabora ikicheza michezo 11 na kukusanya alama 17 kwenye msimamo ikishika nafasi ya 6.