Simba yasitisha mkataba wa CEO wao, yamtaja mrithi wake

Uongozi wa Simba umetangaza kusitisha mkataba na Francois Regis raia wa Rwanda ambaye alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa klabu hiyo.

Regis aliyetambulishwa klabuni hapo Julai 26, 2024 akichukua nafasi ya Imani Kajula, anaondoka akiwa amekaa kwa takribani miezi minne pekee tangu atambulishwe.

Taarifa ya Simba iliyotolewa leo Novemba 23, 2024, imesema: “Tunapenda kuutarifu umma kuwa Klabu ya Simba imefikia makubalino ya kusitisha mkataba na ndugu Francois Regis ambaye alikuwa ni Mtendaji Mkuu kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu. Tunamshukuru Mr. Regis kwa kipindi alichohudumu katika klabu yetu.

“Bodi imefanya uteuzi wa Bi. Zubeda Hassan Sakuru kama Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mkuu.

“Bi.Zubeda yuko mbioni kuhitimu Shahada yake ya kwanza ya Uzamivu, ana Shahada mbili za Uzamili katika Utawala wa Umma kutoka Chuo Kikuu cha Warwick, Uingereza na Chuo Kikuu cha Mzumbe Tanzania. Pia ana Shahada ya kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe.

“Bi.Zubeda amefanya kazi kama Meneja Miradi wa Simba akimsaidia Bw. Kajula kuhusu mchakato wa kutengeneza sera na ushauri wa masuala ya kiutendaji.”

Katika kipindi cha 2015 hadi 2020, Zubeda alikuwa mbunge wa viti maalum kupitia Chadema.

Kwa upande wa Regis, alikuwa CEO wa pili raia wa kigeni kuhudumu ndani ya Simba baada ya Senzo Mbatha kutoka Afrika Kusini ambaye alikaa kwa msimu mmoja wa 2019/20 kabla ya kuhamia Yanga.

Related Posts