Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa angalizo la mvua kubwa kwa maeneo machache ya mikoa minane nchini kesho Novemba 24, 2024.
Taarifa ya TMA iliyotolewa leo Jumamosi Novemba 23, saa 9.30 mchana imeyataja maeneo hayo kuwa ni Nyanda za Juu
Kaskazini Mashariki, mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Mengine yatakayopata mvua ni ya Kati mwa nchi, mikoa ya Singida na Dodoma, na ya Magharibi mwa nchi, mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi.
TMA imesema uwezekano wa mvua hizo kutokea ni wa wastani, huku ikieleza kiwango cha athari zinazoweza kutokea pia ni cha wastani.
Mamlaka imetaja athari zinazoweza kujitokeza ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, hivyo imewataka wazingatie angalizo hilo na kujiandaa.
TMA ilishatoa mwongozo kwa sekta za usafirishaji, mamlaka za miji na menejimenti ya maafa kuchukua tahadhari ya mvua za msimu wa masika.
Sekta nyingine zilizotakiwa kuchukua tahadhari ni za kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, afya na sekta binafsi.
Tahadhari hiyo ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Ladislaus Chang’a Oktoba 31, 2024 katika mkutano na waandishi wa habari, akieleza kuhusu mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka.
Maeneo hayo ni ya kanda za Magharibi, Kati, Nyanda za Juu Kusini Magharibi, Kusini mwa nchi, Ukanda wa Pwani ya Kusini na yaliyopo Kusini mwa Mkoa wa Morogoro.
Alisema maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Singida na Dodoma; kaskazini na mashariki mwa Mkoa wa Lindi na kaskazini mwa mikoa ya Mbeya na Iringa, yatakuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Amesema mikoa ya Njombe, Ruvuma, Mtwara, maeneo ya kusini na magharibi mwa Mkoa wa Lindi, kusini mwa mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro yatapata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Amesema mvua zilitarajiwa kuanza wiki ya nne ya Oktoba katika Mkoa wa Kigoma na ifikapo Novemba itasambaa maeneo mengine yanayopata mvua za msimu, huku Mkoa wa Ruvuma zikitarajiwa kuanza Desemba.
Amesema kipindi cha nusu ya pili ya msimu kati ya Februari hadi Aprili, 2025 kitakuwa na mvua nyingi ikilinganishwa na nusu ya kwanza ya Novemba, 2024 hadi Januari, 2025.