Makundi yatoka kwenye ukumbi wa mazungumzo kwa hasira – DW – 23.11.2024

Nchi za Umoja wa Ulaya, Marekani na mataifa mengine tajiri katika mkutano wa hali ya hewa, COP29 unaofanyika nchini Ezerbaijan, yamekubali kuongeza ufadhili wa hadi dola bilioni 300 ifikapo mwaka 2035 kwa ajili ya kuyasaidia mataifa yanayoendelea kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Maamuzi hayo yamefikiwa baada ya pendekezo la hapo awali la ufadhili wad ola bilioni 250 kupingwa na kuonekana kana kwamba ni kitendo cha dharau.

Soma Pia: COP 29 yaingia katika siku ya ziada Azerbaijan

Muda wa mkutano huo uliokuwa umalizike siku ya Ijumaa uliongezwa ili kuwezesha wajumbe kutoka karibu nchi 200 kufikia makubaliano na kuweza kupitisha maazimio  juu ya mpango wa ufadhili wa hali ya hewa kwa muongo ujao.

Azerbaijan | COP29  Baku
Wanaharakati wa mazingira waandamana BakuPicha: Aziz Karimov/REUTERS

Hata hivyo bado haijawa wazi ikiwa nchi hizo tajiri zimewasilisha rasmi marekebisho kwa nchi zinazoendelea ambazo zimekusanyika katika mji mkuu wa Azerbajan, Baku, na kama marekebisho hayo ya kuongeza fedha za ufadhili yataungwa mkono na nchi zinazoendelea.

Mazungumzo ya awamu hii ya COP29 yameonyesha wazi mgawanyiko kati ya serikali za mataifa tajiri yaliyobanwa na bajeti finyu za ndani na nchi zinazoendelea ambazo zinayumba kutokana na kuongezeka kwa majanga yanayosababishwa na dhoruba, mafuriko na ukame yote hayo yakiwa yanachochewa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Vilevile kushindwa katika siku za nyuma kutimizwa ahadi za kukidhi majukumu ya kifedha ya hali ya hew ani hali inayozifanya nchi zinazoendelea kutoamini ahadi mpya zinazotolewa.

Soma Pia: Guteress awatolea wito viongozi wa G20 kufanikisha mazungumzo ya COP29

Wajumbe kutoka kwenye visiwa vidogo na mataifa masikini siku ya Jumamosi waliondoka katika mashauriano ya hali ya hewa yaliyoongezwa muda kati yao na Azerbaijan ambayo ni rais wa COP29, kwa madai kwamba maslahi yao juu ya fedha yalipuuzwa.

Mwenyekiti wa Muungano wa Nchi za Visiwa Vidogo, vinavyokabiliwa na kupanda kwa kina cha Bahari, Cedric Schuster kutoka Samoa, amesema wamechukua hatua hiyo kwa sababu wanahisi haki haijatendeka na kwamba mapendekezo yao hawakusikilizwa.

Alipoulizwa kama hatua hiyo ya kutoka kwenye mkutano ni mgomo, Waziri wa  mazingira wa Colombia, Susana Mohamed, aliliambia shirika la Habari la The Associated Press kwamba wamefanya hivyo kuashiria kutoridhika kwao.

Nchi zinazoendelea zimezilaumu nchi tajiri kwa kufanya zinavyotaka kwa kuahidi ufadhili mdogo wa kifedha na wakati huohuo kutumia mivutano iliyopo ili kufanikisha wanachotaka.

Mataifa tajiriyana wajibu wa kuzisaidia nchi zilizo hatarini kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo ya mjini Paris mwaka 2015.

COP29  Mkutano wa hali ya hewa
Mkutano wa hali ya hewa Baku, AzerbaijanPicha: Sean Gallup/Getty Images

Mataifa yanayoendelea yanatafuta kiwango cha dola trilioni 1.3 kusaidia kukabiliana na ukame, mafuriko, kuongezeka kwa kuongezeka kwa kina cha Bahari na joto kali, ambapo fedha hizo zinatarajiwa kufidia hasara na uharibifu uliokithiri unaosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, na wakati huo huo fedha hizo pia zitatumiwa kuziwezesha nchi hizo zinazoendelea kubadili mifumo yao ya nishati kwa kuwezesha matumizi ya nishati safi  na kuachana na nishati zinazozalisha hewa ukaa. Makundi kadhaa ya nchi mbalimbali yanadai ahadi kubwa zaidi kutoka kwa mataifa yaliyoendelea kiviwanda na kuchukua hatua Madhubuti juu ya mabadiliko ya hali ya hewa na jurekebisha mienendo yao katika miaka ijayo.

Vyanzo: RTR/AFP/DPA

 

Related Posts