Dar es Salaam. Hospitali ya Aga Khan leo imeadhimisha siku ya watoto njiti ikiweka msisitizo wa kuwepo juhudi za pamoja kuhakikisha huduma bora za utunzaji wa watoto wachanga zinatolewa.
Siku hii ambayo duniani huadhimishwa Novemba 17, hospitali hiyo imeadhimisha leo kwa kuzikutanisha familia zenye watoto waliozaliwa kabla ya muda.
Katika maadhimisho hayo wazazi na walezi walishiriki kwa kutoa shuhuda zao, changamoto walizokutana nazo, furaha ya kuona watoto wao wakikua na kuwa imara, huku msisitizo mkubwa ukiwekwa kwenye upatikanaji wa huduma bora za utunzaji wa watoto wachanga.
Daktari bingwa wa watoto waliozaliwa kabla ya muda, Yaser Abdallah amesema ili kuepuka vifo hivi visivyo vya lazima, kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za utunzaji wa watoto wachanga ni muhimu.
Mbali na hilo amesema ni muhimu kwa familia zilizopata watoto wa namna hiyo kuwa wavumilivu na wenye ujasiri.
“Ingawa maendeleo yamefikiwa katika huduma za utunzaji wa watoto wachanga, familia nyingi duniani bado hazina upatikanaji wa huduma zinazohitajika kwa watoto hao ili wakue kwa afya bora na kuimarika.
“Kila siku, takriban watoto 500 huzaliwa kabla ya wakati nchini Tanzania, na watoto hawa ni wengi kati ya wale wanaofariki ndani ya mwezi mmoja baada ya kuzaliwa,” Dk Abdallah.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan, Tanzania Sisawa Konteh amesema hospitali hiyo imejizatiti kutoa huduma bora kwa watoto hawa waliozaliwa kabla ya wakati.
“Tunasherehekea uvumilivu mkubwa wa watoto hawa na mama zao na baba zao na tunaheshimu timu ya wataalamu wa afya inayofanya kazi bila kuchoka kuwatunza.
“Pia tunaendelea na juhudi zetu za kuongeza uelewa na kusaidia familia katika kila hatua ya safari yao. Tuungane kwa pamoja katika dhamira ya kuwapa watoto hawa maisha yenye afya na mustakabali bora,”amesema Konteh.
Hafla hiyo pia imejumuisha fursa za kutoa elimu kupitia majadiliano kuhusu mustakabali wa huduma za afya kwa watoto wachanga, ambapo wataalamu walitoa mwanga kuhusu uvumbuzi wa kisasa na changamoto katika utunzaji wa watoto wanaozaliwa mapema.