Utetezi wamuokoa na adhabu ya kunyongwa

Moshi. Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, imemhukumu Sifael Kivuyo, kutumikia kifungo cha miaka 18 jela kwa kosa la kumuua bila kukusudia, mwanamume aliyemkuta chumbani na mpenzi wa kike wa mwalimu wake wa uchoraji.

Ndugu yake, Emmanuel Kivuyo alihukumiwa kifungo cha nje katika hatua za awali za kesi baada ya kukiri kosa la kusaidia kuficha taarifa za mauaji hayo, chini ya kifungu 213 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Sifael alishtakiwa kwa kosa la mauaji ya kukusudia, lakini Jaji Lilian Mongella, aliyesikiliza kesi alilishusha kosa hilo hadi kuua bila kukusudia, baada ya utetezi wake kuwa alimuua Rodgers Kessy katika harakati za kujilinda.

Hukumu iliyopatikana kwenye tovuti ya Mahakama Novemba 23, 2024 ilitolewa Novemba 13.

Mahakama imempa faida mshitakiwa licha ya ushahidi wa Jamhuri kudai lengo lilikuwa kumwibia marehemu fedha na pikipiki yake.

Mauaji hayo yalitokea Mei 10, 2021 eneo la Mnazi Shah Tours katika Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro. Mwili wa marehemu ulikutwa na jeraha kubwa kichwani, ambalo polisi walidai lilitokana na kupigwa na nyundo.

Ushahidi wa upande wa mashitaka ulidai mshitakiwa alimuua Kessy katika harakati za kumpora fedha na pikipiki.

Ilidaiwa katika kutekeleza mauaji hayo alitumia waya na nyundo vilivyopokewa kama kielelezo na Mahakama.

Ni ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri kuwa mshitakiwa na Emmanuel Kivuyo, walitaka kuutupa mwili wa Kessy ili kuficha matendo yao.

Utetezi ulioishawishi mahakama

Katika utetezi wake, Sifael Kivuyo alikiri kumuua Kessy lakini akajitetea kuwa alifanya hivyo katika harakati za kujilinda.

Alidai siku ya tukio alikuwa akisafiri kutoka Sanya Juu hadi Moshi kumtembelea mwalimu wake.

Alieleza alipofika eneo la kazi la mwalimu wake huyo Elia Laizer, alimpa ufunguo wa nyumba yake na kumtaka aende kupumzika.

Sifael alidai alipofika, nje ya nyumba alikuta pikipiki imeegeshwa. Alidai alifungua mlango na ndani alimkuta mpenzi wa mwalimu wake aliyekuwa Rodgers Kessy (marehemu) ambaye awali alikuwa hamfahamu.

Alidai mpenzi wa mwalimu wake alitaka kufahamu yeye ni nani, akamweleza ameelekezwa aende hapo kupumzika.

Aliieleza Mahakama mwanamke huyo alisema hamfahamu, hivyo kumtaka aondoke mara moja katika nyumba, vinginevyo angepiga kelele kuwa ni mwizi.

Alidai mwanamume aliyekuwa na mwanamke huyo alianza kumshambulia kwa kutumia kioo, lakini alimsukuma Kessy akaangukia nguzo ya chuma ya kitanda.

Sifael alidai baada ya tukio hilo yeye na mwanamke huyo walikimbia kutoka eneo hilo, yeye alikwenda moja kwa moja kwa mwalimu wake kumweleza kilichotokea.

Mwalimu wake alimtaka abaki eneo lake la kazi pamoja na wafanyakazi wengine ili aende nyumbani kwake, lakini baada ya kitambo kidogo alirudi na pikipiki ya Kessy akawaagiza wafunge ofisi, waende kupumzika.

Katika utetezi alidai mwalimu aliondoka na hakujua alikokwenda lakini siku iliyofuata alimpigia simu akimjulisha kuwa amekamatwa na Polisi na kumwelekeza afike nyumbani kwa mwalimu wake.

Alidai alikwenda kama alivyoelekezwa na akiwa njiani kuelekea nyumba hiyo, barabarani alikuta watu wengi na pembeni kulikuwa na gari la polisi.

Alieleza alimuona mwalimu wake akiwa katika gari hilo akiwa amekalishwa chini.

Alipojitambulisha, polisi walimtaka waende naye kituoni kutoa maelezo.

Sifael alidai alikataa kutoa maelezo kwa sababu alikuwa peke yake, ndipo alipigwa na kulazimishwa kusaini nyaraka.

Baadaye alipelekwa kwa mlinzi wa amani ambako alitoa maelezo akieleza ndiyo yanafanana na kile alichokieleza mahakamani na si polisi.

Katika hukumu yake, Jaji Mongella alisema kwa kuzingatia ushahidi wa utetezi wa mshtakiwa, anaona ni wazi bado anakiri kumuua Kessy na kwamba, katika kesi ya jinai hakuna ushahidi bora kama wa kukiri kosa.

Jaji alisema kwa kuzingatia utetezi wa mshtakiwa kuwa mauaji yalitokana na yeye kujilinda (self defence), swali linabaki ni kama anahusika na mauaji ya kukusudia au akabiliwe na kosa dogo la mauaji ya bila kukusudia.

“Ushahidi wa Jamhuri ni kuwa lengo lilikuwa kumwibia marehemu lakini kwa upande wa pili mshtakiwa anasema aliandika maelezo kwa mlinzi wa amani yanayoeleza kuhusu ‘self defence’ na hakupewa hayo maelezo,” alisema.

Jaji alisema kwa kuzingatia mazingira ya tukio lenyewe la mauaji, anaona mshtakiwa ndiye alisababisha kifo cha Kessy lakini kwa kuzingatia utetezi wake, anamuona hana hatia ya mauaji ya kukusudia bali ya kuua bila kukusudia.

Alisema kwa kuzingatia sababu mbalimbali zilizotokana na maombolezo ya mshtakiwa na rai ya upande wa mashitaka, anamhukumu kifungo cha miaka 18, lakini anaondoa miaka mitatu aliyokaa gerezani hivyo itakuwa kifungo cha miaka 15.

Related Posts