Moshi. Mkazi wa Kata ya Kirua Vunjo Kusini, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Florence Malya (54), amefariki dunia baada ya kudaiwa kushambuliwa na watu waliokuwa wakimtuhumu kuwaibia nondo.
Tukio hilo la kushambuliwa, linadaiwa kutokea Novemba 16, 2024 katika kata hiyo, wakati marehemu na mwenzake, wakifanya biashara yao ya kuuza kuni na alifariki Novemba 17, 2024 wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC).
Akizungumza leo Novemba 23, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa tayari wamewakamata watu wawili kwa tuhuma za kujichukulia sheria mkononi.
“Huyo marehemu na mwenzake wanadaiwa kwenda kuiba nondo, zilikuwa nane kwenye nyumba, wakafurumushwa, yeye akakamatwa, akapigwa, akaletwa polisi akiwa amezidiwa. Tukampeleka hospitali akiwa mtuhumiwa na baadaye akapewa dhamana lakini akafariki,” amesema Kamanda Maigwa.
Ameongeza: “Na yeye alifungua kesi ya shambulio kwa sababu walichukua sheria mkononi kumshambulia na baadaye alifariki, tumekamata watu wawili kuhusiana na tukio hilo.”
Kamanda Maigwa amesema uchunguzi umefanyika na kubainika kuwa marehemu alivunjika mbavu mbili na damu ilivilia kwenye ubongo.
Familia, manusura wasimulia
Akisimulia tukio hilo, Benjamin Moi ambaye alikuwa na marehemu siku ya tukio, amesema walishambuliwa na watu wanne wakiwatuhumu kuiba nondo.
“Siku ya Jumamosi nikiwa na Florence tulipandisha kuni kuuza, jamaa mmoja akatuita, akasema tumpelekee kuni naye anazitaka, tukampelekea akasema tuziweke chini, akauliza bei nikamwambia ni Sh7,000 na mwenzangu Sh2,000, akasema sawa tumsubiri mama amletee hela,” amesimulia Moi.
Ameongeza: “Kidogo tukiwa hapo, tukaona pikipiki moja imekuja, akasema tulieni mama analeta pesa, baadaye ikaja nyingine na ya tatu ikaja na mke wake, tukamwambia tupe basi maana mkeo ameshakuja ili sisi tuondoke zetu.”
Amedai kuwa baada ya watu hao kufika, jamaa huyo alisema anawadai na kuwa wao ni wahalifu na walipohoji, alianza kumshambulia marehemu sehemu mbalimbali za mwili wake hali iliyomsababishia kupata majeraha.
“Alisema tuliiba nondo zake Aprili 2024, wakatupiga baadaye wakatubeba kutupeleka kwa mtendaji lakini hakuwepo, wakaturudisha na kuendelea kutupiga na kutuchoma moto, Jumapili huyu akafariki,” amesema Moi.
Mtoto wa marehemu, Happyness Basil amesema tukio hilo ni la ghafla na gumu kwa familia na kuliomba Jeshi la Polisi kuhakikisha sheria inafuata mkondo wake.
“Tukio hili ni la ghafla na gumu sana kwetu na tumelipokea kwa manung’uniko na majonzi, tunaona baba yetu hakutendewa haki, taarifa tulizozipata ni kwamba mzee alipigwa na watu, natambua hakuna mtu mwenye mamlaka ya kujichukulia sheria mkononi,” amesema Basil.
Amesema: ‘’Naomba polisi na vyombo vya sheria, vihakikishe sheria inafuata mkondo wake, natambua hii ni kesi ya polisi. Tumepokea na limeshatokea hatuna namna ya kuweza kujibu kwa kuchukua sheria mkononi, tunaomba polisi wasimamie sheria ichukue mkondo wake.”