Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amewataka viongozi wa dini ya Kiislamu kuwa karibu na jamii hasa vijana na kuwajenga kimaadili na uzalendo kwa Taifa.
Amesema licha ya viongozi hao kuendelea kufanya kazi nzuri, lakini katika eneo la maadili wanapaswa kufanya shughuli ya ziada ili kudhibiti mmomonyoko uliopo.
Masauni amesema hayo Dar es Salaam leo Novemba 23, 2024 akiwa mgeni rasmi kwenye mkutano wa wanazuoni na masheikh kutoka mikoa mbalimbali waliokutana kupitia kitabu cha Uzalendo na Uislamu.
“Kuna upungufu ambayo mnatakiwa kuufanyia kazi, nataka niwape mifano miwili; wa kwanza kipindi kile cha makundi ya ‘Panya road’ nilibahatika siku moja kwenda Central Polisi hapa Dar es Salaam kuwatembelea vijana waliokamatwa kwa kufanya matukio hayo asilimia kubwa majina yao ni ya Kiislamu,” amesema na kuongeza:
“Mtanisamehe kama nakosea viongozi wangu, takwimu zangu zinaonyesha pia hata shule zetu bado hazifanyi vizuri, sasa huwezi kuwa na jamii nzuri yenye maadili kama haijaandaliwa katika njia zilizonyooka. Halafu nasikia hata kipindi cha mfungo wateja kwenye baa wanapungua sijui ni kweli ingawa sijafanya utafiti.”
Masauni amempongeza mwandishi wa kitabu hicho kinachopitiwa na wanazuoni hao, Sheikh Issa Othman Issa, akiwahimiza viongozi kuihimiza jamii kujenga utamaduni wa kusoma vitabu.
Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir amewataka wanazuoni hao na masheikh kukipitia kitabu hicho kwa makini na kuboresha maeneo watakayoona yana kasoro.
“Mmeitwa na mwandishi kwa kuwa mmeaminiwa, tangulizeni uzalendo pitieni na mmboreshe maeneo yasiyokaa vizuri kwani baada ya kumaliza kitakwenda kushapishwa na kitasomwa na jamii nzima ya Kitanzania, Waislamu na wasio Waislamu,” amesema.
Amewataka masheikh kujenga utamaduni wa kuandika vitabu badala ya kuendelea kukaa kimya na maarifa yao.
“Masheikh wangu mna silica ya kutotaka kuandika vitabu, mnaogopa kukosolewa. Kukosolewa ni jambo la kawaida hakuna mkamilifu, andikeni hata mwenyewe sasa nimeanza kuandika vitabu,” amesema.
Awali, mwandishi wa kitabu hicho, Sheikh Issa Othman Issa amesema amekiandika kitabu hicho akitaka kuondoa dhana ya baadhi ya watu wanaoamini Uislamu na uzalendo ni vitu viwili tofauti.
“Kitabu hiki kimetoa elimu hakuna utofauti wowote Uislamu na uzalendo vinaenda pamoja, nataka kuielimisha jamii ijue na nimewaita masheikh na wanazuoni wapitie na kuboresha pale penye upungufu,” amesema Sheikh Issa ambaye ni mwenyekiti wa Taasisi ya Mwinyi Baraka Foundation.