UNAWEZA kusema Simba imekaa mguu sawa katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara, kwani rekodi zao za matokeo zinazungumza.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara mara 22, kwa sasa ndiyo vinara wa ligi hiyo wakiwa na pointi 28 baada ya kucheza mechi 11, wakishinda tisa, sare moja na kupoteza moja.
Timu hiyo inayonolewa na Kocha Fadlu Davisd, katika mechi tano za mwisho imekusanya pointi 15, ikifunga mabao 10 huku ikiwa haijaruhusu nyavu zao kutikiswa.
Tangu Simba ilipofungwa bao 1-0 na mtani wao Yanga Oktoba 19 mwaka huu, haijapoteza wala kutoka sare katika mechi tano zilizofuatia ikicheza mbili ugenini na tatu nyumbani.
Hatua hiyo imemfanya beki wa kikosi hicho, Shomari Kapombe kutosita kufichua siri iliyopo kupitia matokeo hayo mazuri kwao.
Kapombe ambaye amekuwa beki tegemeo wa kulia ndani ya kikosi hicho msimu huu akifanikiwa kucheza mechi zote 11 kwa dakika 887, amesema matokeo mazuri wanayoyapata yamewaondoa kwenye presha, hivyo sasa wanacheza kwa kujiamini.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kapombe alisema matokeo mazuri wanayoyapata sasa yanawajengea hali ya kujiamini zaodi huku akiamini wachezaji wote wameanza kuelewana.
“Unajua timu ikipata matokeo mazuri inajijenga kiushindani, tofauti na tulivyopoteza mchezo dhidi ya Yanga na kuambulia sare mbele ya Coastal Union na tulikuwa tunakosa utulivu na kutengeneza maelewano mazuri,” alisema na kuongeza.
“Matokeo mazuri ya mechi tano mfululizo yametuondolea presha kwa mashabiki, sasa tunacheza kwa utulivu na kuelekea mchezo wetu wa kwanza hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika naamini tutakuwa kwenye ubora zaidi.”
Kapombe ambaye amefunga bao moja na asisti moja katika ligi msimu huu, alisema licha ya Simba kuwa katika mpango wa kujenga timu kutokana na usajili wa wachezaji wengi wapya uliofanyika sambamba na benchi la ufundi kuwa jipya, lakini matokeo hayo yanaondoa dhana ya ujenzi wa timu.
“Wachezaji wengi walioongezwa wana uwezo mkubwa, kilichopo ni kuisoma ligi yetu na kuingia taratibu kwenye mfumo kitu ambacho tayari kimeanza kuonekana, tumecheza mechi 11, tumepoteza mchezo mmoja na sare moja, ukiangalia sisi ndio timu pekee ambayo tumeruhusu mabao machache ambayo matatu huku tukifunga mechi 22,” alisema na kuongeza.
“Timu ikichanganya zaidi huku tukicheza kwa kuelewana naiona Simba ikiwa bora na ya ushindani tofauti na sasa.”
Kwa sasa Simba inajiandaa na mchezo wa kwanza wa Kundi A katika Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravos Do Maquis ya Angola utakaochezwa Novemba 27 mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kapombe amebainisha, baada ya juzi kutoka kuichapa Pamba Jiji bao 1-0 ugenini katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, sasa akili zao wamezielekeza kwa Bravos kuhakikisha wanaanza vizuri hatua ya makundi.
“Baada ya kumaliza mchezo wetu na Pamba sasa tunaelekeza akili zetu zote kimataifa mchezo ambao ni muhimu kwetu kuhakikisha tunapata matokeo mazuri kwenye uwanja wetu wa nyumbani, tutaingia kwenye mchezo huo tukiwa imara katika kuziwania pointi tatu,” alisema Kapombe.
MATOKEO SIMBA MECHI 5 ZILIZOPITA
Tanzania Prisons 0-1 Simba