KAMA mechi za kuwania kucheza Fainali za Mataifa Afrika (Afcon 2025) zingekuwa na tuzo ya kipa bora, basi nafasi kubwa ingetua kwa Djigui Diarra baada ya kufanya balaa akimfunika hata Andre Onana wa Manchester United.
Diarra ambaye ni kipa namba moja wa Yanga na Timu ya Taifa ya Mali, kwenye mechi sita alizoiongoza Mali kufuzu Afcon 2025 amemaliza na clean sheet 5 akiwa kinara akiruhusu bao dhidi ya Msumbiji mchezo wa sare ya bao 1-1 nyumbani.
Mali ilimaliza kinara Kundi I ikishinda mechi nne na sare mbili huku ikiwa haijapoteza mechi yoyote na imeruhusu bao moja pekee.
Nyuma ya Diarra, yupo kipa Dimitry Bertaud anayekipiga Montpellier ya Ufaransa na alicheza mechi tano na kupata clean sheet nne akiifanya DR Congo kumaliza kinara wa Kundi H wakikusanya jumla ya pointi 12, huku akiruhusu bao moja dhidi ya Guinea, huku mechi ya mwisho waliyofungwa 2-1 na Ethiopia akidaka Lionel M’Pasi N’Zau.
Makipa wengine wenye clean sheet nne ni Onana (Cameroon), Mohamed El-Shenawy (Misri) na Adilson Neblu (Angola).
Onana alisaidia Cameroon kumaliza kinara Kundi J ikikusanya pointi 14 akiruhusu mabao mawili kwenye mechi sita alizocheza.
Mohamed El-Shenawy anayeichezea Al Ahly, aliisaidia Misri kumaliza kinara wa Kundi C wakivuna jumla ya pointi 14 sawa na Adilson Neblu wa Desportivo 1º de Agosto akilisaidia taifa lake kumaliza kinara kwenye Kundi F nao wakikusanya pointi 14.
Akizungumzia kiwango cha Diarra, Kocha wa Mali, Tom Saintfiet alisema kwenye safu ya ulinzi ya timu hiyo kipa huyo ni nguzo muhimu akiendeleza rekodi yake ya ubora.
Saintfiet ambaye ni kocha wa zamani wa Yanga, alisema Diarra ni kipa wa daraja la juu na ni bahati mbaya pekee inayomfanya kucheza soka la Afrika akisema ana ubora wa kuwa kipa bora hata Ulaya.
“Ni vile anacheza hapa Afrika lakini kwangu mimi na tutakubaliana hata kwa wengine wanaomjua ni kipa ambaye alitakiwa kucheza Ulaya, ana ubora wa kufanya mambo makubwa akiwa langoni.
“Hapa Mali ukiangalia moja ya nguzo muhimu kwenye safu ya ulinzi ni yeye (Diarra) ni kipa ambaye hata timu ikifanya makosa mnakuwa na imani kuna mtu nyuma atawarudisha mchezoni,” alisema kocha huyo.