Wawili mbaroni kwa kuvunja vioo vya treni SGR kwa mawe

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limewakamata na kuwahoji watuhumiwa wawili kwa kosa la kuharibu kwa kuvunja vioo viwili vya treni ya Mwendo Kasi (SGR) kwa kutumia mawe.

Tukio hilo limetokea mchana wa Novemba 22, 2024 katika Kijiji cha Manase Wilaya ya Chamwino jijini Dodoma treni hiyo ilipokuwa ikipota ikitokea jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi iliyotolewa jana, baada ya tukio hilo, Jeshi lilifanya msako na kufanikiwa kuwakamata Erasto Michael Richard,(16) na Hassan Ndahani (12) wote wakazi wa Kijiji cha Manase.

“Chanzo cha kufanya uharibifu huo ni baada ya kuona treni ikipita wakarusha mawe kwa pamoja ili kuona kama yataweza kushindana na mwendo wa treni,” imeeleza taarifa hiyo ya Polisi. 

Jeshi hilo limetoa wito hasa kwa wananchi wanaoishi maeneo ambayo treni ya kisasa inapita kuendelea kupeana elimu juu ya umuhimu wa kulinda miundombinu ya usafiri huo kwani upo kwa ajili ya manufaa ya wote.

“Aidha, kila mzazi/mlezi ana wajibu wa kutoa elimu kwa familia hasa watoto kuacha vitendo ambavyo vitasababisha uharibifu kwa reli na treni ya kisasa, kwani itawasababisha kukinzana na sheria za nchi,” imeelekeza taarifa hiyo.

Hata hiyo ikumbukwe Novemba 11 kwa mujibu wa taarifa ya Polisi jijini Dodoma liliwakamata watuhumiwa wawili wakazi wa Kilosa kwa tuhuma za kuhujumu miundombinu ya reli ya mwendokasi.

Tukio hilo lilitokea Oktoba 3, mwaka huu saa tano usiku katika kijiji cha Msagali, Wilaya ya Mpwapwa jijini humo, ambapo watuhumiwa wanadaiwa kukata na kuiba waya wa shaba (copper wire) katika madaraja matatu ya reli hiyo.

Piaa, Jeshi liliwashikilia watuhumiwa wanne kwa nyakati tofauti kwa tuhuma za kuharibu na kuiba miundombinu ya Serikali kwa kukata nyaya za shaba katika mradi wa treni ya umeme SGR wilaya ya Bahi.

Related Posts