Ubunifu ni uwezo wa kufikiri, kutafuta majibu, au kutatua changamoto kwa namna isiyotarajiwa.
Unamsaidia mtu kupambana na changamoto zake kwa namna nyepesi, bila ubunifu ni vigumu kwa mtu kuendana na mabadilikotunayokabiliana nayo kila siku yanayohitaji majibu mapya.
Maandiko mbalimbali kuhusu masuala ya malezi yanaeleza kuwa ubunifu ni uwezo unaotegemea mazingira ya kimakuzi anayokutana nayo mtoto.
Miongoni mwa maandiko hayo ni lile lililoandikwa katika tovuti ya ParentMap, ambayo hutoa mada mbalimbali kuhusu masula ya malezi.
Katika makala yake iliyobebwa na kichwa cha habari ‘Secret to Raising a Creative Child’ inaeleza kuwa kila mtu ana uwezo wa kuwa mbunifu katika mambo mbalimbali anayoyafanya.
Hata hivyo, inabainisha kuwa changamoto ni namna gani mtu anaweza kutumia uwezo huo wa ubunifu uliopo ndani yake kuleta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Inafafanua kuwa kumfanya mtu aweze kutumia uwezo huo uliobarikiwa hautokei tu, bali huanza kuandaliwa kutokana na aina ya malezi na makuzi anayopatiwa mtoto.
Kwa sababu hiyo, jamii inahitaji kujifunza namna ya kujenga uwezo huo kwa watoto.
Akizungumza na Mwananchi, mtaalamu wa malezi kutoka Shirika linaloshughulikia masuala ya watoto na malezi la Bright Jamii Initiative, Irene Fugara anasema mzazi anaweza kumtengenezea mazingira mtoto wake ambayo yatamchochea kuwa mbunifu.
Anasema anaweza kumtengenezea mazingira hayo kupitia nyanja mbalimbali, ikiwamo ya michezo anayocheza.
Anaongeza kuwa ni vyema kujiuliza kama aina ya michezo anayocheza mtoto wako inamsaidia kujifunza na kumuandaa kuwa mbunifu.
“Baadhi ya wazazi huwa wananunua tu vitu vya kuchezea watoto bila kuzingatia ni kwa kiasi gani vinamsaidia mtoto huyo kujifunza masuala mbalimbali muhimu, kwa ajili ya ukuaji wake,” anasema na kuongeza:
“Ni muhimu pia kuzingatia aina ya vifaa anavyotumia mtoto wako katika michezo hiyo kama inamsaidia kujifunza masuala mbalimbali yaliyopo katika jamii kulingana na umri wake.”
Lakini pia anasema ni muhimu kumhimiza mtoto kuwa na muda wa kila siku wa kufanya kazi zinazochochea ubunifu, kama vile kucheza michezo ya kufikirika au kufanya kazi za mikono sambamba na kuchora picha za aina mbalimbali.
Anagusia pia suala la ushiriki wa mzazi katika shughuli mbalimbali ambazo zinamsaidia mtoto kujifunza na kumuandaa kuwa mbunifu, akibainisha baadhi ya mambo kama ya uchongaji, uandishi wa hadithi, au uundaji wa vitu mbalimbali.
“Kitendo hicho ni muhimu, kwani kinamsaidia kumuandaa mtoto kuwa na ushirikiano na wenzake na kufanya kazi kama timu,” anasema Fugara.
Mtaalamu huyo anasema mzazi pia anapaswa kumhamasisha mtoto kuuliza maswali na kutoa nafasi ya kujifunza kwa kupitia majibu yake mwenyewe.
Anasema kwa kufanya hivyo, kutamsaidia mtoto kufikiria kwa kina na kuwa na mbinu za kutatua matatizo.
“Mzazi anapaswa kumfundisha mtoto kuwa makosa ni sehemu ya mchakato wa kujifunza, hivyo kuwa na ujasiri wa kujaribu mambo mapya bila hofu ya kushindwa,” anasema.
Akizungumza na Mwananchi katika mashindano ya kukuza ubunifu katika masuala ya teknolojia na uhandisi kwa watoto yanayojulikana kama Pan African Steam, yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Young Engineers Tanzania, Benazir Kurji anasema ni muhimu kwa mtoto kuanza kutengenezwa kuwa mbunifu tangu akiwa na umri mdogo.
Kurji anasema hiyo ndiyo sababu iliyowasukuma wao kama taasisi kuona wana wajibu wa kulitekeleza hilo kupitia kufanya mashindano yanayolenga kukuza ubunifu katika mnasuala ya teknolojia na uhandisi kwa watoto yanayojulikana kama Pan African Steam.
Mashindano hayo yalifanyika Novemba 16, 2024 katika Ukumbi wa Shule ya Msingi Aga Khan na kuwakutanisha wanafunzi takribani 200 kutoka nchi tatu za Afrika Mashariki, ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda.
Anasema kwa mwaka huu shindano hilo linafanyika kwa mara ya pili na liliwahitaji washiriki kutumia vifaa mbalimbali vya michezo ya watoto walivyopewa kubuni mfano wa mji wa kisasa wenye maeneo yote muhimu. ikiwemo njia kuu za usafirishaji.
“Washiriki hao walitakiwa kutumia takribani dakika 50 kutekeleza wazo hilo wakiwa katika makundi ya watoto takribani sita,” anasema.
Akifafanua madhumuni ya mashindano hayo, Kurji anasema ni kuwafundisha watoto ujuzi muhimu, hasa katika karne hii ya 21 iliyotawaliwa na teknolojia katika kila nyanja.
Pia kuanza kuwajenga watoto katika fikra za kibunifu na uvumbuzi na kufanya kazi kwa ushirikiano.
“Ndiyo maana limelenga zaidi watoto kuanzia umri wa miaka 6-14 ili kuanza kuwajengea uwezo na kuwapatia ujuzi tangu wakiwa na umri mdogo,” anasema.
Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Aga Khan, Blandina Duwe, anasema kuwa mashindano haya ni muhimu kwa sababu inawasaidia wanafunzi kutumia ujuzi wao kutatua matatizo mbalimbali ya jamii ili kuleta maendeleo endelevu.
“Tunachokifanya sasa hivi ni kuendeleza pale Serikali ilipoanzia kwamba tuna mipango ya maendeleo mbalimbali inayotokana na jumuiya ya dunia nzima.
Sasa hawa watoto wetu wanapata fursa ya kubuni vitu mbalimbali ambavyo vinaweza kuisaidia jamii katika kutatua matatizo kama miundombinu, foleni za barabarani, vyote hivi vinaweza kusaidia kutatua matatizo haya,” anasema.