Sekta binafsi yakosolewa kwa ukosefu wa elimu juu ya madhara ya kemikali

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), George Katabazi, amesema sekta binafsi bado haijatimiza wajibu wake wa kutoa elimu kwa wafanyakazi na jamii kuhusu madhara ya kemikali hatarishi na jinsi ya kuepuka athari zake.

Katabazi ameyasema hayo Novemba 23, 2024, jijini Dodoma wakati wa kufunga kampeni ya kutoa elimu juu ya usafirishaji salama wa kemikali hatarishi, hususan sodiam sayanaidi. “Watanzania wengi hawana elimu kuhusu kemikali hii. Ni muhimu tuendelee kuwapatia elimu,” amesema.

Ameongeza kuwa matumizi ya kemikali ni muhimu katika sekta za afya, kilimo, viwanda, maji, na madini. Hata hivyo, alisema baadhi ya kampuni hazitekelezi takwa la kisheria la kutoa elimu kwa wafanyakazi na jamii, akisisitiza hatua zichukuliwe dhidi yao. “Sekta binafsi bado ni changamoto kubwa katika hili,”.

Katabazi aliweka wazi kuwa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani Na. 3 ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake za mwaka 2020 zilitungwa kulinda afya na mazingira. Alisisitiza kuwa utoaji wa elimu ni mojawapo ya masharti ya msingi yanayopaswa kutekelezwa na serikali pamoja na sekta binafsi.

Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Daniel Ndiyo, alisema mamlaka hiyo imekuwa ikitoa mafunzo kwa makundi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wachimbaji wadogo wa dhahabu na madereva wa kemikali.

Kwa upande wake, Joseph Mbanga, kiongozi wa usafirishaji kutoka Kampuni ya Barrick, aliipongeza kampeni hiyo kwa kuimarisha ushirikiano kati ya polisi na kampuni zao katika kuhakikisha usalama wa usafirishaji wa kemikali.

Kampeni hiyo ilianza Novemba 14, jijini Dar es Salaam na kufungwa leo jijini Dodoma.

Related Posts