Walichokifanya ‘’Mdundo’ wadau wa muziki wafunguka “elimu itolewe, vipato viongezeke”

WADAU wa mziki nchini wamesema upo umuhimu wa wasanii wa mziki nchini kupatiwa elimu ya uwekezaji ili iwasaidie kutumia vizuri vipato vyao vinavyotokana na kazi hiyo hasa pale shughuli zao hizo zinapofikia ukomo.

 

Walitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam, katika hafla iliyowakutanisha wasanii hao kwa ajili ya kuwapatia elimu ya namna ya kutumia mifumo ya kidijitali kusambaza maudhui, iliyoandaliwa na Mdundo.Com.

 

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Benki ya CRDB, Emmanuel Kiondo, alisema ipo mifano ya wasanii wengi ambao walifanikiwa kutengeneza fedha nyingi kupitia kazi hiyo lakini baadae walirudi kuwa masikini baada ya kukumbwa na matatizo.

 

“Na hii yote inatokana na kukosekana kwa elimu ya fedha, kwamba msanii anakuwa na wakati mzuri, anafanya kazi na kutengeneza fedha lakini badala ya kuwekeza, anatumia vibaya na mwisho wa siku anapokuja kupoteza uwezo wake wa kufanya shughuli yake hiyo anakufa masikini.

 

“Mtu badala ya kuwekeza fedha yake anayoipata kwa jasho, anaitumia vibaya katika mambo yasiyo ya msingi na akipata matatizo anapotea au wakati mwingine hata inaidi kumchangia. Kwa hiyo sisi kama CRDB, tunawapatia elimu ya namna ya kuwekeza kile wanachokipata, tunataka waache mambo ya kizamani,”alisema Kiondo.

 

Mdau mwingine wa muziki, Aman Martin, alisema kuna haja ya kuongeza uelewa kwa wasanii wa mziki na wanaowasimamia ili wafahamu namna ya kutumia vizuri mifumo ya kidijitali katika kusambaza kazi zao.

 

Alisema bado kuna ugeni mwingi wa namna ya kutumia mifumo ya kidijitali katika kusambaza maudhui kwa wasanii wengi na kwamba kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha wana kuwa na  taarifa na maarifa ya kutosha ili iwasaidie kuepukana na shida ya kufanya kazi isiyo na manufaa.

 

“Tuachane na zile stori ambazo tumekuwa tukikutana nazo sana, kwamba mtu fulani alisaini mkataba ambao haukuwa na masilahi kwake, au mwingine hata hajui ni sehemu gani sahihi aiendee,”alisema Martin.

 

Alisema bila kujali ni maarufu au laa, msanii akitumia vizuri mifumo ya kidijitali kusambaza maudhui ya kazi yake, ni rahidi kunufaika.

 

“Cha msingi ni wanamziki hao kufahamu namna mifumo hiyo ya kidijitali inavyoendeshwa na namna ya kuitumia katika kuinua au kutangaza kazi zao,”alisema Martin.

 

Maureen Njeri, Mkurugenzi Mkazi wa Mdundo.Com, alisema wao wamerahisisha kazi kwa  kuwaunganisha wasanii wa muziki kutoa maudhui yanayofaa na kuyasambaza kwenda kwa jamii kwa lengo la kuhakikisha kila mmoja wao ananufaika na kazi hiyo.

 

“Na tunatoa kipaumbele kwa muziki wa nyumbani, hasa kwa nyimbo zinazoimbwa kwa lugha ya kiswahili, kwa hiyo tunatoa nafasi kwa wasanii kuitumia vema fursa hii,”alisema Maureen.

 

Related Posts