Kaya maskini milioni 1.2 kunufaika bima ya afya kwa wote

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dk. Irene Isaka amesema wanatarajia kuzilipia bima familia milioni 1.2 zisizokuwa na uwezo wa kumudu gharama za bima ya afya kwa wote.

Ametoa kauli hiyo Novemba 22,2024 wakati wa mjadala kuhusu utekelezwaji wa Sheria na Kanuni za Bima ya Afya kwa Wote ulioandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA).

Amesema kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wamezitambua familia milioni 3.5 na kwa kuanzia wataanza na familia milioni 1.2.

“Tumejipanga kutoa huduma kwa Watanzania wote, tangu Oktoba mwaka huu tumeanza kuwashirikisha wadau kuhusu Bima ya Afya kwa Wote na tunatarajia hadi kufikia Januari 2025 tutakuwa tumewafikia wadau wote,” amesema Dk. Isaka.

Naye Naibu Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk. Grace Maghembe, amesema wameboresha miundombinu ya utoaji huduma za afya ili kuwawezesha wananchi kupata huduma maeneo ya karibu.

Amesema wamejenga vituo na zahanati 980, hospitali mpya za wilaya 29, wamejenga ICU 21, mitambo 28 inayozalisha hewa tiba, wameongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba na kufikia asilimia 70 na kwamba juhudi hizo zimewezesha asilimia 77 ya Watanzania kupata huduma za afya karibu.

Aidha amesema ndani ya miaka miwili wamenunua magari ya kubeba wagonjwa 600 na kwa mwaka huu wameajiri watumishi 10,000.

“Tumeongeza usimamizi wa rasilimali fedha, vifaa tib ana vingine na tunatumia teknolojia kufika maeneo ambako madaktari au wauguzi hawajafika,” amesema Dk. Maghembe.

Akizungumzia taarifa ya utendaji wa Soko la Bima kwa mwaka 2023, Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini, Dk. Baghayo Saqware, amesema sekta ya bima imeendelea kukua na mchango katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 1.99 mwaka 2022 na kufikia asilimia 2.01 mwaka 2023.

Aidha amesema ajira katika sekta hiyo zimeongezeka kutoka 4,173 mwaka 2022 na kufikia 5,595 mwaka 2023.

Kuhusu madai ya bima na madeni amesema yaliyolipwa yameongezeka kutoka Sh milioni 389 hadi Sh milioni 488.2 huku madeni nayo yakiongezeka kutoka Sh bilioni 1.077 na kufikia Sh bilioni 1.4.

Balozi wa Bima, Japhet Hasunga ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Vwawa, Japhet Hasunga, amesema nguvu kubwa inapaswa kuwekezwa kwenye elimu ili kuzuia kasi ya magonjwa hasa ya kuambukiza ambayo yamekuwa yakigharimu fedha nyingi kuyatibu.

“Sehemu kubwa ambayo tunatakiwa kuwekeza kwa kiwango kikubwa ni kuzuia watu kupata magonjwa na kutoa elimu, watu wajue nini kifanyike kwenye afya zao na uwepo utaratibu mzuri wa kuhakikisha sekta binafsi inashirikishwa ipasavyo,” amesema Hasunga.

Akizindua ripoti hiyo Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande, ameitaka mamlaka hiyo kuendelea kuweka juhudi ili kupata mafanikio makubwa zaidi.

“TIRA na wadau wengine endeleeni kuimarisha mifumo ya kidigitali, msimamie miongozo mliyotoa kuhakikisha wananchi wanapata huduma zilizokusudiwa kwa haki na kwa haraka,a wapate haki zao bila ubaguzi wa aina yoyote,” amesema Chande.

Related Posts