MSHAMBULIAJI wa Mtibwa Sugar, Raizin Hafidh ameziingiza vitani Kagera Sugar na Pamba Jiji ambazo zimeonyesha nia ya kuihitaji saini ya nyota huyo, dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa rasmi Desemba 15, mwaka huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Raizin mwenye mabao manane na kikosi hicho, alisema ni kweli timu hizo zinamhitaji ingawa hawezi kuzungumza chochote juu ya hilo, kwani bado ana mkataba wa mwaka mmoja aliousaini ili kukirejesha Ligi Kuu Bara.
“Ni kweli nimekuwa na ofa nyingi lakini sijafanya maamuzi yoyote hadi sasa, naheshimu mkataba niliokuwa nao hapa Mtibwa na kama itatokea ishu nyingine mashabiki zangu watajua, ninachojua nina deni kubwa ambalo napaswa kulitimiza,” alisema.
Licha ya kauli ya nyota huyo ila Mwanaspoti linatambua kwamba, Raizin ni miongoni mwa washambuliaji wanaohitajika na Kagera Sugar, ili akaungane na aliyekuwa kocha wake Mmarekani, Melis Medo ambaye ameonyesha kumuhitaji kuungana naye.
Raizin aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Dodoma Jiji huku akiwahi kuzichezea Gwambina na Coastal Union alisema anawaomba mashabiki waendelee kuwaunga mkono ili kuirejesha Mtibwa Ligi Kuu, kwani bila ya wao hawatofikia malengo hayo.