Mtanzania aoga minoti CAF | Mwanaspoti

LICHA ya FC Masar anayoichezea Winga Mtanzania, Hasnath Ubamba kumaliza nafasi ya tatu Ligi ya Mabingwa kwa wanawake, lakini nyota huyo ameondoka na medali na minoti.

Mchezo huo ulitamatika dakika 90 kwa sare ya bila kufungana na Masar kushinda kwa mikwaju ya penati 4-3 dhidi ya Edo Queens.

Ligi hiyo ilishirikisha timu nane kutoka kanda mbalimbali za Afrika iliyoanza Novemba 9 na fainali kufanyika Novemba 23, Morocco.

Masar ilianza makundi kwa kuitandika bingwa mtetezi Mamelodi Sundown Ladies kwa bao 1-0, ikatoka 0-0 na Edo na kisha kumaliza makundi kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya C.B.E iliyowapa tiketi ya kutinga nusu fainali ikitolewa kwa mabao 2-1 na AS Far.

Akiwa Mtanzania pekee aliyecheza michuano hiyo tangu hatua ya makundi hadi nafasi ya tatu kwa dakika zote 90, hajaondoka patupu akibeba medali ya mshindi wa tatu na minoti kwa chama lake hilo kuondoka na Dola 350,000 sawa na Sh875 milioni, huku bingwa akiondoka na Sh1.5 bilioni na mshindi wa pili Sh1 bilioni.

Akizungumza baada ya michuano hiyo, Ubamba alisema; “Nashukuru ndoto yangu ya kwanza kucheza nje imetimia, pili kushiriki michuano mikubwa ya CAF tena nikianza, sina mengi zaidi ya kushukuru.”

Masar ndio mara ya kwanza kushiriki michuanohiyo na kuweka historia ya kuifunga bingwa mtetezi Mamelodi kabla haijatolewa hatua ya makundi.

Related Posts