Wiki hii nzima, nimekuwa jijini Dodoma kuhudhuria mikutano mitatu muhimu ya mambo ya habari. Tulianza na mkutano mkuu wa 13 wa mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dotto Biteko.
Ukaja mkutano wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba na Ijumaa tukaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Habari, mgeni rasmi akiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Ijumaa iliyopita ilikuwa ni Siku ya Uhuru wa Habari duniani. Je, kuna uhuru wa habari bila uhuru wa kiuchumi wa vyombo vya habari au waandishi wa Habari? Mtu mwenye njaa anaweza kuwa huru? Vyombo vya habari vyenye njaa inayomtegemea mtoa habari kwa usafiri na waandishi wa habari wenye njaa na umasikini uliotopea kiasi cha kutegemea zile bahasha, wanaweza kuwa huru?
Waziri Mkuu, Majaliwa aliwataka viongozi na watendaji wa Serikali waondoe ukiritimba kwenye suala la upatikanaji wa habari ili kuwawezesha wanahabari kupata taarifa sahihi na kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Namnukuu: “Viongozi na watendaji wa Serikali na mashirika zingatieni Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa ya mwaka 2016 na ondoeni ukiritimba katika suala la upatikanaji wa habari ili wanahabari wawezeshwe kupata taarifa sahihi na wafanye kazi zao kwa ufanisi wa hali ya juu.”
Haki ya kupata habari iko kwenye Ibara ya 18(1) na (2) ya Katiba inayosema: (1) Kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati. Kifungu cha (2): Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii, hivyo haki ya kupata habari ni haki muhimu inayotolewa na Katiba yetu.
Japo sheria ya upatikanaji taarifa imefungua milango ya upatikanaji habari ni haki, lakini ukiritimba kwenye kanuni za utumishi wa umma kuhusu utoaji habari bado uko pale pale. Kila wizara, idara, na taasisi zina vitengo vya habari, na vina wasemaji, lakini wasemaji hao ni kama zuga tu, kama matarishi, badala ya kuwa wasemaji rasmi wa taasisi zao, wengi ni watoa taarifa tu, yaani press release, kwa vile kikanuni wasemaji rasmi wa taasisi ni watendaji wakuu wa taasisi hizo na sio wasemaji.
Ukiritimba huu upo kuanzia kwa msemaji wa Ikulu, kazi ya Msemaji wa Ikulu ilikuwa ni kutoa tu press release na siyo kusema. Pongezi nyingi ziende kwa msemaji wa sasa wa Ikulu, Zuhura Yunus, siyo tu anatoa press release, anasema na vipindi pia anatengeneza. Hiki Kinachofanywa na Zuhura kifanywe na wasemaji wengine wote wa Serikali, wasiishie kutoa press release.
Lazima kila wizara, idara, taasisi, zaidi ya utoaji wa habari, ziwe na vipindi vya uelimishaji umma. Nashauri huu ukirimba wa utoaji habari, uondolewe kwenye kanuni, wasemaji wa Serikali waisemee Serikali na taasisi zake.
Tuna mihimili mitatu rasmi ya Serikali, Bunge na Mahakama, na mhimili wa nne usio rasmi ni vyombo vya habari. Mihimili hii mitatu inapewa fedha, inaangaliwa vizuri na inaheshimiwa, lakini huu mhimili wa nne wa vyombo vya habari, kiukweli uko kama mtoto yatima, hakuna anayejali.
Kitu muhimu cha kwanza kwa nchi yetu ni mwananchi, ndiye mwenye nchi, mwenye Katiba na mwenye kila kitu. Ni mwananchi kupitia kura yake ndiye anamuajiri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile mihimili yote mitatu. Ni kwa kupitia kodi yake ndiye anawalipa mishahara yao wote, kuanzia mshahara wa Rais na Serikali yake yote na mihimili yote na kutoa fedha za kuendesha serikali na kugharimia kila kitu, lakini kwa nini huu mhimili wa nne umeachwa kama mtoto yatima?
Kwa mwananchi, ni mhimili gani ni muhimu zaidi kwake kati ya Serikali, Bunge, Mahakama na vyombo vya habari?
Wakati nikiishi Uingereza, niliajiriwa na taasisi ya FCO ya Uingereza, kwenye stakabadhi ya malipo ya mshahara wangu, nilijikuta nakatwa fedha zinaitwa Radio Levy, kwa ajili ya kugharamia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC). Pia, kuna kodi ya “TV Set”.
Nilimfuata mtu wa utawala, nikamwambia “mimi kwangu sina redio, wala sisikilizi BBC, na hata kama ningekuwa nayo, ningesikiliza RTD na sio BBC, hivyo naomba kwenye slip yangu nisikatwe Radio Levy wala TV Set”. Ndipo nikaambiwa malipo hayo ni lazima yalipiwe, uwe unasikiliza BBC au husikilizi, ili mradi uko Uingereza na unaingiza mapato, una wajibu wa kugharimia vyombo vya habari.
Sisi Tanzania, pia tuna malipo ya lazima ya kugharimia mambo mbalimbali, mfano kwenye mafuta, umeme, maji. Tunatoa ruzuku kwenye maeneo mengi tu, ikiwemo ruzuku kwa vyama vya siasa, nani muhimu kati ya vyombo vya habari na vyama vya siasa hadi kustahili ruzuku?
Ili kuwapatia Watanzania haki yao ya msingi ya kupata habari, ufike wakati tuanzishe tozo ya vyombo vya habari ili huu mhimili wa nne nao ugharamiwe kama ile mihimili mitatu.