BEKI wa FC Lupopo, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ amesema wameanza vizuri msimu kwenye ligi licha ya kutolewa mapema michuano ya Ligi ya Mabingwa na Bravos ya Angola kwa jumla ya mabao 3-1 ugenini na nyumbani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ninja alisema hadi sasa wako nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi A ikiwa na pointi 15 baada ya mechi sita na licha ya ugumu wa ligi ya Congo, lakini mwenendo wa timu hiyo uko vizuri kwani wanatofautiana pointi moja na TP Mazembe inayoongoza ligi ikiwa imecheza michezo saba.
“Tunaendelea kupambana hadi sasa tuko salama, lakini bado ligi ndiyo kwanza imeanza, naamini mwenendo huo unatupa kujiamini kwenye mechi zijazo,” alisema Ninja.
Kuhusu jeraha lake alisema, “Niliumia goti mwezi uliopita nikiwa mazoezini, lakini sasa naendelea vizuri na muda si mrefu nitarejea uwanjani.”