‘607 wanahitaji upandikizaji ini Muhimbili’

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), imeeleza kuwa itaanza upandikizaji wa ini ifikapo mwaka 2025.

Hatua hiyo ya Muhimbili inakuja wakati ambapo kuna wagonjwa 607 wanaohitaji upandikizaji wa ini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumapili, Novemba 24, 2024 Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi amesema tayari wameanza matayarisho kuelekea upandikizaji wa ini, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya kutoa huduma za ubingwa bobezi nchini.

Naye bingwa mbobezi wa upasuaji wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini na bingwa wa upasuaji kupitia tundu dogo, Dk Kitembo Salumu amesema, mpaka sasa takwimu za hospitali hiyo zinaonyesha kuna zaidi ya wagonjwa 5,000 wenye shida kwenye ini.

Amesema kati yao 2,333 wana uvimbe kwenye ini na 607 wamegundulika kuwa na tatizo la saratani ya ini, wengine maini yamesinyaa hivyo wote wanahitaji huduma ya kupandikizwa ini ambao gharama yake nje ya nchi ni kubwa.

Kwa mujibu wa Dk Kitembo matibabu pekee kwa waliogundulika na saratani ya ini pamoja na ini kusinyaa ni upandikizaji, ingawa wagonjwa wenye uvimbe na changamoto tofauti na hizo wanaweza kutibiwa kwa tiba nyingine wakapona.

Kwa mujibu wa Profesa Janabi, kuanza upandikizaji lengo ni kusogeza huduma hizo karibu na wananchi ambazo hazikuwepo kutokana na kutokuwepo wataalamu, vifaa vya uchunguzi au miundombinu stahiki ya kutolea huduma hizo, hivyo kuigharimu Serikali fedha nyingi kupeleka wagonjwa hao kutibiwa nje ya nchi.

“Gharama ya upandikizaji ini nje ya nchi ni kati ya Dola za Marekani 25,000 hadi 27,000 (sawa na Sh66.4 milioni hadi 71.7 milioni) na fedha hizi zinajumuisha upandikizaji wa ini, kukaa hospitali na matibabu yote kwa mgonjwa na anayechangia ini,” amesema.

Profesa Janabi amesema MNH imeingia makubaliano na hospitali mbalimbali duniani zenye ujuzi huo ili kuanza matayarisho kwa kushirikiana na wataalamu wazalendo, ili  kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa mwaka 2025 Tanzania inaanza kutoa huduma hiyo, kwani miundombinu stahiki ipo na vifaa tiba vya uchunguzi.

“Wiki hii tumeshirikiana na wataalamu kutoka Hospitali ya Fortis ya nchini India ambao wamekua na madaktari wetu kwa siku tatu wameona wagonjwa zaidi ya 100 wenye changamoto mbalimbali za magonjwa ya ini na kutathmini hali ya upatikanaji wa dawa, miundombinu ya maabara na eneo la  uangalizi maalumu (ICU) ambalo linakidhi mahitaji ya huduma hiyo,” amesisitiza Profesa Janabi.

Kwa upande wake bingwa mbobezi wa upandikizaji ini, Dk Gaurav Gupta kutoka Hospitali ya Fortis na Jenifer Choudhary na Mkurugenzi wa Biashara kutoka Vaidam Health wamesisitiza kuwa watatoa ushirikiano na utaalamu unaohitajika kuhakikisha MNH inafikia lengo la uanzishwaji wa huduma hiyo, hapa nchini.

Related Posts