Dar es Salaam. Timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’ imeangukia katika kundi C la fainali za mataifa ya Afrika kwa wanawake (Wafcon) 2024 zitakazofanyika Morocco mwakani, ambalo linaundwa na timu tatu zenye uzoefu na historia nzuri na mashindano hayo.
Timu hizo tatu pinzani za Twiga Stars kwenye fainali hizo za Wafcon ambazo zitafanyika kuanzia Julai 5 hadi Julai 26 mwakani zikishirikisha timu 12 ni Afrika Kusini “Banyana Banyana’, Ghana ‘Malkia Weusi’ na Mali ‘Majike ya Tai’.
Afrika Kusini, Ghana na Mali zipo katika 10 bora kwenye chati ya viwango vya ubora wa soka kwa wanawake barani Afrika kwa mujibu wa viwango vya ubora wa soka vilivyotangazwa na shirikisho la mpira wa miguu duniani (Fifa) mwezi Agosti ambapo Afrika Kusini ipo nafasi ya pili, Ghana ikiwa nafasi ya tano na Mali inashika nafasi ya tisa.
Wakati wapinzani wake wote wakiwepo kwenye 10 bora, Twiga Stars yenyewe ipo nafasi ya 27 katika chati ya viwango vya ubora kwa soka la wanawake Afrika.
Timu ya taifa ya wanawake ya Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’ ndio mabingwa watetezi wa Wafcon na kabla ya fainali zilizopita, walishika nafasi ya pili katika fainali za 2018.
Banyana Banyana imeshiriki mara mbili fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake na mara ya mwisho ilikuwa ni 2023 ilipoishia hatua ya 16 bora.
Timu ya taifa ya wanawake ya Ghana ‘Black Queens’ imeshiriki mara tatu fainali za kombe la dunia kwa wanawake ambapo zote iliishia hatua ya makundi. Iimeshiriki mara 12 tofauti katika fainali za Wafcon ambapo mafanikio yao makubwa ni kumaliza katika nafasi ya pili mwaka 1998, 2002 na 2006 huku ikiishia katika nafasi ya tatu mara tatu ambazo ni 2000, 2004 na 2016.
Mali haijawahi kushiriki fainali za Kombe la Dunia lakini imecheza Wafcon mara saba zilizopita na mafanikio yao makubwa yalikuwa ni kumaliza katika nafasi ya nne katika fainali za 2018.
Ikumbukwe hii ni mara ya pili kwa Twiga Stars kushiriki Wafcon ambapo ya kwanza ilikuwa ni 2010 ilipoishia hatua ya makundi, ilipomaliza ikiwa na pointi moja iliyoipata katika mechi tatu.
Kocha wa Twiga Stars, bakari Shime alisema kuwa wapo tayari kupambana na wapinzani wao hao.
“Timu zote zilizofuzu mashindano hayo ni nzuri na ngumu hivyo sisi tulikuwa tayari kucheza dhidi ya timu yoyote ambayo tungepangwa nayo kundi moja. Tunawaheshimu wapinzani wetu kwenye kundi lakini hiyo haiwezi kututoa kwenye mstari na malengo ni kufanya vizuri,” alisema Shime