Baum atamani kuichezea Twiga Stars

KIUNGO wa Humburger FC inayoshiriki Ligi ya Wanawake Ujerumani, Bundesliga Women, Lisa Baum amesema bado anaamini anaweza kuichezea timu ya taifa ya Wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’.

Nyota huyo aliyeichezea timu ya taifa ya Ujerumani U-20 kwenye michuano ya Kombe la Dunia 2022, alizaliwa Dar es Salaam Tanzania na akizungumza na moja ya vyombo vya Habari, alisema ni Mtanzania halisi ambaye hajakata tamaa kuichezea timu ya taifa.

“Ni kweli nimezaliwa Tanzania mwaka 2006, Dar es Salaam na ndipo pamenikuza kimalezi mpaka mama yangu alipoamua kutuchukua familia nzima tukaja Ujerumani, nikasoma shule za kawaida nikiwa Dar lakini baba yangu ni Mjerumani.”

“Kuhusu kuchezea Twiga Stars niliwahi kufuatwa na viongozi wa huko ili nije kucheza lakini muda ulikuwa si rafiki, tayari nilikuwa nimechaguliwa kuchezea Timu ya Taifa ya Ujerumani chini ya Miaka 20 ambayo ilikuwa ikijiandaa kucheza Kombe la Dunia kwa Wasichana, walikuja muda ambao nimeshafanya maamuzi ya kuitumikia Ujerumani.”

“Naipenda Tanzania na siwezi kusema sitoichezea siku za mbeleni, kwa sababu mambo hubadilika na lolote linaweza kutokea, bado sijachezea timu ya wakubwa ya Ujerumani hivyo nafasi bado ipo kama nikihitajika tena sitopinga.”

Mbali na hilo Baum ni mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha Humburger FC ambacho kipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa Bundesliga na pointi 19 ikiiacha Bayern Munich mkiani ikiwa na pointi sita.

Licha ya kucheza nafasi ya beki, yupo kwenye 10 bora za wafungaji akitupia kambani mabao matatu kwenye mechi 10.

Related Posts