KOCHA Mkuu wa Mbeya Kwanza, Emmanuel Masawe amesema licha ya mwenendo mzuri wa timu hiyo hadi sasa ila bado amewataka washambuliaji wa kikosi hicho kuongeza umakini wa kufunga, kwa sababu nafasi zinapopatikana huwa hazijirudii mara mbili.
Akizungumza na Mwanaspoti, Masawe alisema kwa hivi karibuni kumekuwa na maendeleo mazuri ya utumiaji wa nafasi japo bado wana kazi kubwa ya kufanya ili kusogea juu ya msimamo, huku akieleza ushindani umekuwa ni mkubwa hasa mechi za ugenini.
“Ligi bado inaendelea na tuna michezo mingi ambayo imebaki hivyo tutaendelea kurekebisha mapungufu tuliyoyaona, mabao 10 tuliyoyafunga katika mechi 10 sio mwenendo mzuri na tunapaswa kubadilika kwa haraka ili kujiweka nafasi nzuri,” alisema.
Kikosi hicho chenye maskani yake Mtwara, tayari kimecheza michezo 10, hadi sasa na kati ya hiyo kimeshinda mitano, sare mitatu na kupoteza miwili kikiwa kimefunga mabao 10 na kuruhusu sita, kikishika nafasi ya sita na pointi zake 18.
Masawe anapigania timu hiyo ili iweze kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushiriki msimu wa 2021-2022 kisha kushuka daraja, huku akikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa Mtibwa Sugar, Geita Gold, TMA na Songea United zilizopo juu yao.