Kampeni chafu zinavyoweza kupunguza mwamko wa wapiga kura

Dar es Salaam. Katika kila uchaguzi, sauti ya mwananchi ni msingi wa maamuzi ya kitaifa na mustakabali wa kizazi kijacho.

Hata hivyo, kampeni chafu zimezidi kuwa kikwazo cha wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato huo wa kidemokrasia.

Kampeni chafu, zenye mwelekeo wa kushusha hadhi za wagombea, kueneza taarifa za uongo, na kuchochea hisia za chuki, zimegeuka silaha hatari inayochafua mchakato wa uchaguzi na kuleta madhara makubwa kwa mwamko wa wapiga kura. 

Kampeni chafu ni mbinu zinazotumiwa na baadhi ya wanasiasa au wafuasi wao ili kudhoofisha ushindani wa kisiasa kwa njia zisizo za kimaadili.

Taarifa za uongo na propaganda ni miongoni mwa kampeni chafu.

Kusambaza habari za uongo kuhusu wagombea au vyama pinzani. Mfano ni tukio la uchaguzi wa Marekani mwaka 2016 ambapo habari za uongo zilienezwa kupitia mitandao ya kijamii, na ripoti ya Pew Research Center ya mwaka 2017 ilionyesha  asilimia 64 ya wapiga kura walikumbana na taarifa zenye utata mtandaoni.

Udhalilishaji wa kutumia maisha binafsi ya wagombea kama silaha ya kisiasa badala ya kuzingatia sera zao.  

Chuki za kikabila na kidini husababisha mgawanyiko wa kijamii kwa kutumia kauli za chuki zinazolenga makundi maalumu. 

Haya yote yanachangia siyo tu kupoteza mvuto wa uchaguzi bali pia kuharibu mshikamano wa kitaifa na kudhoofisha demokrasia. 

Kupunguza imani ya wapiga kura kwa mfumo wa uchaguzi. Takwimu za Shirika la International IDEA za mwaka 2022 zinaonyesha asilimia 30 ya wananchi katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, waliripoti kupungua kwa imani yao katika chaguzi kutokana na kampeni chafu.

Wananchi wanapoona wagombea wakitumia mbinu hizi, wanahisi kuwa uchaguzi si jukwaa la mabadiliko, bali ni mchezo mchafu wa kupigania madaraka. 

Kujenga mazingira ya hofu na kukata tamaa

Wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019, ripoti ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Taifa (INEC) ilibaini baadhi ya wapiga kura walikosa kushiriki kutokana na mazingira ya hofu yaliyosababishwa na kampeni za maneno ya uchochezi.

Hofu hii inawafanya wananchi, hasa wanawake na vijana, kujiepusha na kushiriki katika uchaguzi. 

Kuharibu ajenda za maendeleo

Badala ya kujadili sera, kampeni chafu huzingatia masuala yasiyo na tija. Kwa mfano, ripoti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 2021 ilionyesha kampeni za 2020 zilijikita zaidi kwenye masuala binafsi ya wagombea badala ya ajenda za maendeleo, na hili liliathiri upatikanaji wa wapiga kura wenye uelewa wa masuala ya msingi. 

Kampeni chafu si jambo geni. Nchini Kenya, uchaguzi wa mwaka 2007 ulishuhudia machafuko makubwa baada ya kampeni zilizosheheni chuki za kikabila.

Ripoti ya Human Rights Watch (2008) ilionyesha  kampeni hizo zilisababisha vifo vya watu zaidi ya 1,100 na kuathiri takribani milioni 1.2 kwa namna moja au nyingine. 

Kwa Tanzania, uchaguzi wa mwaka 2015 ulishuhudia ongezeko la matumizi ya mitandao ya kijamii kwa ajili ya kampeni, kadhalika ulileta changamoto za habari za uongo zilizoathiri maamuzi ya wapiga kura, kama ilivyobainishwa na ripoti ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) mwaka 2016. 

Demokrasia ni zaidi ya kushinda uchaguzi ni kuhusu kujenga imani na mshikamano.

Kampeni chafu huchochea mgawanyiko kati ya wananchi na kuwafanya wagombea kuonekana si viongozi wa kuaminika bali watu waliotayari kutumia njia yoyote kufanikisha malengo yao binafsi. 

Ripoti ya Afrobarometer ya mwaka 2023, imeonyesha asilimia 54 ya Watanzania wanaamini kuwa wanasiasa hawajali maslahi ya wananchi na kampeni chafu zina mchango mkubwa katika mtazamo huu. 

Shirika la UNDP mwaka 2021, limependekeza kuimarisha elimu ya uraia kwa wapiga kura ili waweze kutambua propaganda na kuepuka kushawishiwa na habari za uongo.

Hii inaweza kufanywa kupitia programu za redio, televisheni, na mitandao ya kijamii. 

Kuzingatia maadili ya kampeni 

Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ina jukumu la kusimamia maadili ya kampeni.

Tamisemi inapaswa kuhakikisha kuwa kila mgombea anazingatia kanuni za maadili za uchaguzi. 

Ushiriki wa asasi za kiraia

Asasi hizi zinaweza kusaidia kufuatilia na kuripoti kampeni chafu. Ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ya mwaka 2022 ilibaini asasi hizo ziliweza kufichua zaidi ya visa 100 vya kampeni zisizo za kimaadili nchini. 

Mitandao ya kijamii kuwajibika

Kampuni zinazomiliki mitandao ya kijamii, kama Facebook na Twitter, zinapaswa kuwa na udhibiti wa maudhui yanayosambazwa, kuhakikisha kuwa taarifa za uongo na propaganda zinadhibitiwa haraka. 

Kampeni chafu ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya kidemokrasia na mwamko wa wapiga kura.

Ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa chombo cha mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, ni lazima jamii, serikali, na vyama vya siasa kushirikiana kwa karibu kuondoa hali hii.

Demokrasia bora inahitaji maadili, mshikamano, na heshima sifa ambazo kampeni chafu haziwezi kutoa. 

“Katika kila uchaguzi, tunapaswa kuangalia mbali zaidi ya ushindi wa kisiasa, tukizingatia mshikamano wa taifa letu,” aliwahi kusema Rais wa kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Mandela. 

Ni wakati sasa wa kuchagua njia bora, ili kuhakikisha kwamba wapiga kura wanahisi kuwa sehemu ya mabadiliko badala ya kuwa wahanga wa siasa chafu.

Kila kura ina thamani, na kila mwananchi ana wajibu wa kuilinda demokrasia dhidi ya uchafuzi wa kampeni zisizo na tija. 

Related Posts