Pointi 15 zampa kiburi Sillah

Nyota wa Azam FC, Gibril Sillah, ameweka wazi siri ya mafanikio ya timu yake kufanikisha ushindi wa mechi tano mfululizo katika Ligi Kuu Bara, akisema kuwa matokeo hayo yametokana na juhudi za kila mchezaji na marekebisho ya mapungufu yaliyojitokeza katika mechi za awali. 

Sillah alizungumza baada ya Azam kuvuna pointi 15 katika ushindi wa mechi dhidi ya Namungo (1-0), Tanzania Prisons (2-0), Kengold (4-1), Yanga (1-0) na Kagera Sugar (1-0).

Ushindi huo umeifanya Azam kufikisha pointi 24 baada ya michezo 11, wakiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi nyuma ya Simba SC, wenye pointi 28 lakini wakilingana pointi na Yanga. 

“Tulipoteza dhidi ya Simba na kutoa sare na Mashujaa, jambo ambalo lilituonyesha wapi tulikosea. Kila mchezaji alijituma, tulisikiliza maelekezo ya benchi la ufundi, na kufanyia kazi mapungufu yetu. Huo ndio msingi wa ushindi huu wa mechi tano mfululizo,” alisema Sillah mwenye mabao mawili.

Sillah pia aliongeza kuwa mchezo wao dhidi ya Yanga ulikuwa wa kihistoria kwa Azam, kwani ushindi dhidi ya mabingwa watetezi wa ligi ulikuwa na maana kubwa kwa morali ya timu. 

“Kila mechi ni ngumu, lakini ushindi dhidi ya Yanga ulikuwa maalum. Umetupa nguvu ya kuamini kuwa tunaweza kushinda dhidi ya timu yoyote ikiwa tutafuata mipango yetu,” aliongeza. 

Akizungumzia mchezo ujao dhidi ya Singida Black Stars utakaochezwa Novemba 27 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Sillah alisema timu iko tayari kukabiliana na changamoto mpya. 

“Singida Black Stars ni timu bora, na tunajua haitakuwa mechi rahisi. Tunahitaji kuendelea kuwa makini, kujituma na kuhakikisha tunapambana kwa dakika zote 90 ili kupata ushindi,” alisema. 

Azam FC, chini ya kocha Rachid Taoussi, imeonyesha kiwango bora msimu huu, na mafanikio yao ya hivi karibuni yamewaweka kwenye mbio za ubingwa. Mechi dhidi ya Singida Black Stars, walioko nafasi ya tatu na pointi 23, inatarajiwa kuwa kipimo kingine muhimu kwa vijana hao wa Chamazi.

Related Posts