Jamii yang’atwa sikio kuwakumbuka wenye mahitaji

Dar es Salaam. Kampuni, taasisi na wadau nchini wamekumbushwa kuwa na desturi ya kurudisha kwa jamii,  ili kurejesha tabasamu kwa watu wenye mahitaji wakiwemo wagonjwa, watoto yatima na wazee wasiojiweza.

Kundi hilo ambalo mbali na mahitaji ya chakula, mavazi, sabuni, mafuta linahitaji pia furaha inayotokana na kutembelewa pamoja na kushikwa mkono na watu wanaowazunguka.

Rai hiyo imetolewa hii leo Jumapili, Novemba 24, 2024 na Ofisa Masoko wa Kampuni ya nywele ya Prima Afro, Jackline Mputa wakati akikabidhi mahitaji ya watoto katika kituo cha kulelea watoto yatima na wanaoishi mazingira hatarishi cha New Faraja kilichopo Mburahati Dar es Salaam.

Ameyasema hayo baada ya kukabidhi vyakula, mafuta na taulo za kike na mahitaji kwa watoto katika kituo hicho chenye watoto takribani 91.

“Nawaomba watu wenye uwezo, kampuni wawe na tabia ya kusaidia jamii kwa chochote walichonacho kwa sababu jamii ndo inafanya tuwe hapa,” amesema na kuongeza:

“Tuwe na tabia ya kutembelea maeneo tofauti tofauti kuona changamoto walizonazo na kuwasaidia kwasababu inarejesha furaha na kuona wanakumbukwa,” amesema Mputa.

Amesema itengwe desturi ya kugawana na jamii hata kwa mwaka mara moja kampuni yeyote ile inayotegemea jamii ikifanya hivyo changamoto zinazokabili kundi hilo zinapungua na kuisha kabisa.

“Awali tumefanya usafi na tumekabidhi vifaa vya usafi vya ndani na nje katika Hospitali ya Mwananyamala ili kusaidia katika kutunza mazingira ya hapo,” amesema.

Mlezi wa kituo hicho Karima Baraka amesema watu wanapaswa kuhamasishwa kutoa kwenye vituo kama anacholelea watoto kwa sababu kujitolea kwao kuwalea kunapunguza hatari inayoweza kuwakumba wakiwa mitaani.

“Kuna watoto hawana kabisa wazazi hapa na mtu akija hapa hata kucheza nao wanapata furaha na wanafarijika wanajisikia wako na dada shangazi au mjomba,” amesema.

Akizungumzia mahitaji waliyopelekewa ameshukuru kampuni ya Prima Afro kwa kuwakumbuka. Amesema imeleta faraja hata kwao walezi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Happy Times Salon, Salema Lema amesema mahitaji waliyoyatoa kwa kushirikiana na Prima Afro, yanaonesha nia ya kuthamini mchango wa jamii.

Amesema mahitaji yakitolewa kwenye vituo vya wenye mahitaji vitapunguza changamoto walizonazo huku akisisitiza watu kuwakumbuka.

Mmoja ya watoto wa kituo hicho Amina Shaban (Si jina halisi) ameshukuru huku akiomba watu kutembelea kwa ajili ya kucheza nao.

Related Posts