Mgunda alia na straika wake

LICHA ya uwepo wa mshambuliaji mkongwe, Meddie Kagere, Kocha wa Namungo FC, Juma Mgunda ameweka wazi mipango yake ya kusajili mshambuliaji mpya dirisha dogo la usajili linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 15 na kufungwa Januari 15.

Mgunda amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha safu yao ya ushambuliaji ambayo, kwa sasa, inakosa makali ya kutumia nafasi nyingi wanazozitengeneza. 

Akizungumza baada ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mashujaa FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Jumamosi, Mgunda alikiri safu yake ya ushambuliaji inakabiliwa na changamoto kubwa ya umaliziaji, jambo ambalo limeathiri matokeo yao msimu huu.

Namungo imepoteza michezo nane kati ya 11 iliyocheza hadi sasa, kuonyesha kuwa kocha huyo anatakiwa kusajili mshambuliaji, imefunga mabao matano tu na kuruhusu 13 kwenye michezo hiyo.

“Tuna wachezaji wenye uwezo mzuri, lakini hatutumii nafasi tunazozipata. Hii ni changamoto kubwa. Kwa sasa tunatakiwa kuendelea na mapambani wakati ukifika tutaliangalia hilo ikiwa ni pamoja na kuboresha maeneo mengine,” alisema Mgunda.

Namungo, ambayo kwa sasa inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu kati ya timu 16, imejikusanyia pointi tisa pekee baada ya mechi 11. Katika mechi hizo, imeshinda michezo mitatu. 

Kagere, mshambuliaji aliyewahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akiwa na Simba SC, ameweza kufunga bao moja tu msimu huu, hali ambayo imezidi kuleta presha kwa safu ya ushambuliaji ya Namungo. 

Mgunda aliongeza kuwa, licha ya changamoto hizo, bado anaamini timu yake ina uwezo wa kubadilisha mwelekeo wa matokeo yao kwa kuongeza nguvu kupitia usajili sahihi. 

Huku dirisha dogo likikaribia, mashabiki wa Namungo wanatarajia kuona timu yao ikiongeza nguvu itakayorejesha matumaini ya kubaki kwenye ligi na kuleta ushindani unaotarajiwa.

Related Posts