Huduma za afya zaanza kuimarishwa maeneo yaliyoathiriwa na tabia nchi

Dodoma. Wakati Mkutano wa 29 wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) ukiendelea mjini Baku, Azerbaijan, taasisi isiyo ya kiserikali ya Elico Foundation imeimarisha juhudi zake za kuboresha huduma za afya kwenye baadhi ya maeneo ya mikoa ya Kigoma na Dodoma iliyopata athari ya mabadiliko ya tabianchi.

Mradi huu ulianzishwa kufuatia utafiti uliofanywa na Elico Foundation kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef).

Kwa mujibu wa Meneja Mradi wa Elico Foundation,  Fredrick Mushi, utafiti ulibaini changamoto katika utoaji wa huduma za afya ya msingi kwenye maeneo ya vijijini, hususan yale yanayokabiliwa na ukame wa mara kwa mara na yale yanayokumbwa na mafuriko.

Mushi amesema kutokana na matokeo hayo, taasisi hiyo ilianza kutekeleza mradi wa kuimarisha huduma za afya kwa lengo la kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa makundi haya yaliyo hatarini zaidi.

“Mradi huu umefadhiliwa na Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania, ambao umechangia takribani Sh1.5 bilioni kufanikisha utekelezaji wake,” amesema Mushi.

Amesema awamu ya kwanza ya mradi huo inatekelezwa katika wilaya nne za Chemba na Mpwapwa mkoani Dodoma, Kasulu na Buhigwe mkoani Kigoma.

“Tumelenga mikoa ya Dodoma na Kigoma kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Dodoma ina changamoto ya ukame na uhaba wa maji, inahitaji zahanati zenye miundombinu thabiti ili kukabiliana na changamoto hizi sambamba na Kigoma, ingawa sio kama Dodoma,” amesema.

Amesema mradi pia unalenga kusaidia zahanati katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

 “Kwa sasa, tunajiandaa kuanza awamu ya pili ya mradi huu. Katika Mkoa wa Dodoma, tutaongeza wilaya tatu mpya za Kondoa, Kongwa na Chamwino, wakati kwa Mkoa wa Kigoma, mradi utaendelea katika wilaya za Uvinza na Kibondo,” aliongeza.

Mradi huo unalenga kuboresha huduma za afya kwa kushughulikia changamoto za ukame na mafuriko ambazo zimeathiri ustawi wa jamii katika maeneo haya. 

Mushi amesema mradi huo unaofahamika kama Kijanisha Afya, ulioanza Novemba 2023 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi ujao na umejikita katika kuboresha huduma za afya vijijini kupitia ufungaji wa mifumo ya umeme wa sola, upatikanaji wa usafiri, na uimarishaji wa huduma za maji katika zahanati ambazo hazina miundombinu ya kutosha. 

Mushi amesema kwa awamu ya kwanza, mradi ulilenga kuboresha zahanati 16, lakini kutokana na uhitaji mkubwa, idadi iliongezeka hadi zahanati 18.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chemba, Marco Mgonja amesema mradi wa umeme wa sola na maji safi kwenye zahanati umeleta mabadiliko katika huduma za afya, hasa kwa akina mama wajawazito.

Awali, zahanati hiyo kwa kutokuwa na umeme ilikuwa ikitegemea taa za chemli na jiko la mafuta, hali iliyoleta changamoto kubwa katika utoaji huduma.

“Kwa sasa, umeme wa sola umeimarisha huduma za usiku, kuhifadhi chanjo, na kuendesha vifaatiba, huku kisima cha maji safi kikiwezesha usafi wa mazingira na kupunguza magonjwa ya maambukizi.

“Mradi pia umeleta pikipiki na baiskeli za umeme zinazosaidia watumishi kufikisha huduma kwa jamii za pembezoni kwa gharama nafuu,” alisema.

Tabibu wa zahanati ya Kijiji cha Makamaka, Akwilina Dobey, amesema umeme wa sola umeimarisha huduma za usiku, huku kisima cha maji kikihudumia zahanati, wakazi zaidi ya 3,000, na mifugo kijijini.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Baraka Samson, alithibitisha kuwa changamoto zilizotolewa kuhusu zahanati ya Kijiji cha Makamaka zitafanyiwa kazi.

Mkurugenzi Mtendaji wa ELICO Foundation, Sisty Basil, alisema taasisi yake itatoa taa kubwa kuongeza mwanga maeneo ya nje ya zahanati na baadhi ya vifaatiba muhimu kama vipimo vya mkojo na wingi wa damu mwilini.

Basil pia aliwataka wananchi kutunza miundombinu ya umeme na maji kwenye zahanati hiyo.

Mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, Bahati Mohamed, alieleza kuwa umeme wa sola utasaidia mama wajawazito kupata mwanga wa kutosha wakati wa kujifungua, jambo ambalo lilikuwa vigumu awali kutokana na utegemezi wa taa za tochi.

Related Posts